Muungano mkuu wa upinzani nchini Misri , wa National Salvation Front, leo umetoa wito wa kupiga kura ya "hapana" dhidi ya rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo kwenye upigaji wa kura ya maoni hapo Disemba 15.
Pamoja na hapo mwanzo kukataa kushiriki kwenye kura hiyo, sasa muungano huo wa upinzani umetaka watu washiriki kwa kuikataa rasimu hiyo na pia umetaka upewe uhakika juu ya uendeshaji wa kura hiyo.
Muungano huo umedai kuwa kura hiyo ya maoni iliyopangwa kufanyika Jumamosi isimamiwe na majaji kwa jumla na kuangaliwa na makundi ya ndani na nje ya asasi zisizokuwa za kiserikali. Wamedai pia vituo vya kupigia kura pia vinapaswa kuwa na ulinzi wa kutosha.
Hamdeen Sabahi mjumbe wa ngazi ya juu wa muungano huo ameonya katika mkutano na waandishi habari kuwa iwapo uhakikisho huu hautatiliwa maanani, muungano huo utajitoa katika kupiga kura.
Wakati huo huo juhudi za kutatua mzozo wa kisiasa nchini Misri ambao unazidi kuwa mbaya, zimepata pigo leo wakati jeshi lilipoahirisha ghafla mazungumzo yaliyokuwa yawakutanishe wapinzani na serikali, licha ya hapo kabla wapinzani kukubali kushiriki.
No comments:
Post a Comment