HATIMAYE
msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi ya kuua
bila kukusudia amerejea uraiani jana baada ya kuachiwa kwa dhamana na
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Lulu
anakabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven
Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu. Aliachiwa kwa
dhamana jana saa 9:56 alasiri, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa
ametimiza masharti.
Hadi
anaachiwa kwa dhamana jana saa 9:55 alasiri, msanii huyo alikuwa
ameshakaa mahabusu kwa miezi tisa, tangu alipokamatwa kwa tuhuma hizo,
Aprili 7, 2012.
Aliachiwa
baada ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Francis Kabwe kukagua na
kuridhishwa na nyaraka muhimu zilizohitajika kama sehemu ya masharti ya
dhamana na kutoa amri kwa msanii huyo kuachiwa huru kwa dhamana.
Dhamana hiyo
ilitolewa juzi lakini msanii huyo hakuweza kutoka gerezani kutokana na
Msajili wa Mahakama aliyepaswa kuthibitisha vielelezo vya dhamana hiyo
kutokuwepo mahakamani.
Akizungumza
huku akitokwa machozi muda mfupi baada ya kuachiwa, Lulu alimshukuru
Mungu, mawakili wake na watu wote waliokuwa wakimwombea katika mapito
yake hayo.
“Nawashukuru
watu wote. Watu waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu lakini kesi bado
ni safari ndefu. Nawashukuru watu wote waliokuwa pamoja nami,
namshukuru Mungu kwani yeye ndiye kila kitu,” alisema Lulu.
Mmoja wa
mawakili wake, Peter Kibatala aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano
katika kufanikisha dhamana hiyo... “Sisi mawakili pamoja na Lulu
mwenyewe tunaishukuru sana Mahakama kwa kufanikisha haki hii ya msingi.
Msajili ametusubiri hadi sasa na hatimaye mchakato huu umetimia.”
Hali ilivyokuwa mahakamani
Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.
Alipofikishwa,
alipelekwa katika mahabusu na baada ya takriban saa moja, aliingizwa
katika Ofisi ya Naibu Msajili, Kabwe huku akiambatana na wakili wake,
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, wadhamini wake wawili na askari
Magereza.
Kabwe
alipitia masharti yote ya dhamana ikiwamo wadhamini wawili waliosaini
bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Bondi hiyo iliwekwa na Florian James
Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Dk
Verusi Mboneko Kataruga wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Saa 9:26
alasiri alitoka katika ofisi hiyo na kurudishwa mahabusu ya mahakama
hiyo kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za kimahakama na za
Jeshi la Magereza na baadaye aliingizwa masjala ya makosa ya jinai kwa
ajili ya kusaini hati ya dhamana.
Baada ya
hapo, alitoka nje ya masjala hiyo na kutoa shukrani kwa waandishi wa
habari, ndugu na jamaa waliojitokeza mahakamani kisha kuondoka
mahakamani hapo kwa gari aina ya Toyota Landcruiser.
Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, Aprili 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
Picha zaidi angalia hapa chini
Dr. Cheni ( Big Brother wa LULU) amekuwa mstari wa mbele toka mwanzo hadi leo
Hapa LULU akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuwa huru, Dr Cheni na mama LULU walikuwa karibu nae
OMG..... Familia ni kitu kingine , Mama na LULU akikumbatiana na Mwanawe huku wakilia kwa furaha
Wakili wake akiongea na wanahabari
LULU aliondoka na gari hii kuelekea nyumbani
Habari na James Magai na Vicky Kimaro
Chanzo - Mwananchi
Picha - kishymba blog
No comments:
Post a Comment