Kesi ya kusikiliza ombi la kuachiwa kwa dhamana bingwa wa michezo ya
Olimpiki ya walemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius, imeahirishwa
hadi Jumatano ili kutoa muda kwa waendesha mashitaka kupitia hati ya
maelezo.
Hatua hiyo inatokana na waendesha mashitaka kutaka muda zaidi kusoma
maelezo yaliyowasilishwa na upande wa utetezi. Awali kesi hiyo ilipokuwa
ikisikilizwa leo mshitakiwa alisema hakudhamiria kumuua mpenzi wake
mwanamitindo, Reeva Steenkamp. Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo ya
Oscar Pistorius, ambaye ameshtakiwa kwa tuhuma za kumuuwa mpenzi wake
kwa kudhamiria. Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama ya mjini Pretoria
kuwa Pistorius alimpiga risasi mpenzi wake mara nne.Mwendesha mashtaka, Gerrie Nel, aliiambia mahakama kuwa Pistorius alifyatua risasi kupitia kwenye mlango wa kuingilia bafuni katika nyumba yenye ulinzi mkali na kumuua mpenzi wake mwanamitindo, Reeva Steenkamp, aliyekuwa na umri wa miaka 26. Mwendesha mashtaka huyo pia aliiambia mahakama kwamba mlango wa kuingilia bafuni ulikuwa umevunjwa.
Mwendesha mashtaka alisema, wakati Pistorius akiwa anatoa machozi ya kimya kimya, kwamba mshtakiwa, Pistorius, aliinuka kutoka kitandani na kuipachika miguu yake ya bandia, na alianza kutembea kiasi cha umbali wa mita saba kutoka chumbani, kuelekea bafuni na kufyatua risasi.
Dhamira ya mauwaji
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama kwamba Pistorius aliua kwa kudhamiria kwa sababu tokea mwanzo alipanga kusema kwamba alifikiri alikuwa anamuua mwivi. Mwendesha mashtaka, Gerrie Nel, aliiambia mahakama kuwa Pistorius alipanga kila kitu mapema, na aliuliza kwani nini mwivi ajifungie bafuni?
Lakini wakili wa Pistorius, Barry Roux, ameyakana mashtaka ya kuua kwa kudhamiria. Wakili huyo aliiambia mahakama kwamba ufyatuaji wa risasi ulikuwa ni tukio la ajali na wala siyo mauaji. Wakili huyo amesema hakuna ushahidi wa mauaji.
Mshatakiwa Pistorius alifikishwa mahakamani mjini Pretoria leo kusikiliza uamuzi wa mahakama iwapo anaweza kuachiwa kwa dhamana. Akitetea hoja ya mteja wake kuachiwa kwa dhamana, wakili Barry Roux alisema kuwa Pistorius, mwenye umri wa miaka 26, hana mashtaka mengine yanayomkabili. Mwanamichezo Pistorius, anayetumia miguu bandia katika kukimbia, mwaka jana alikuwa mtu wa kwanza aliyekatwa miguu yote miwili kushiriki katika mashindano ya michezo ya olimpiki.
Shughuli za maziko zafanyika
Wakati kesi ya Pistorius ikiendelea katika mji wa Pretoria, aliyekuwa mpenzi wake, Reeva Steenkamp, alikuwa anafanyiwa maziko katika mji wa Port Elizabeth. Mwili wake ulipelekwa kwenye kanisa dogo. Jeneza lake lililopambwa kwa maua lilibebwa na watu sita na kupelekwa kwenye sehemu ya kuchomwa moto. Watu waliokuwa wamejawa majonzi waliwasili kwenye maziko yaliyokuwa ya faragha katika mji wa Port Elizabeth.
Marehemu, aliyekuwa msanii wa kuonyesha mitindo na aliyekuwa anasomea sheria, alikuwa na umri wa miaka 29. Aliuawa siku ya wapendanao, Valentine's Day - Februari 14. Mama yake, June Steenkamp, amesema anataka kujua kwa nini ameuliwa? Mama huyo aliuliza kwa nini Pistorius alifanya hivyo? Wakati huo huo wataalamu wa sheria wamesema kuwa kesi ya Pistorius ambayo imeahirishwa itachukua muda mrefu.
HABARI NA DW SWAHILI
No comments:
Post a Comment