Saturday, April 27, 2013

HII MAKA LA ALIYOANDIKA LEMA AKIELEZEA UKWELI WA TUKIO ZIMA KUHUSU FUJO ZILIZOTOKEA CHUONI ARUSHA KABLA YA KUTIWA MBARONI


 


Majira ya saa nne asubuhi 24/04/2013 nilipokea taarifa kutoka Chuo cha Uhasibu juu ya tukio la mauaji ya mwanafunzi yaliyotokea jana usiku kwa kuchomwa kisu eneo karibu na chuo , nilipita Chuoni hapo baada ya kusikia taarifa hiyo , nilikuta
Wanafunzi wengi sana wakiwa wamekusanyika pamoja wakiwa na jazba huku Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilaya akijaribu kuwasihi watulie wakati walipokuwa wanatafuta muafaka wa kuzuia jazba ambayo ilikuwa ina lengo la kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa.

Nilipata faragha ya kuongea na Mwalimu aliyekuwa pale ( Dean of Student ) pamoja na OCD na wote walinieleza tatizo lilivyoanza na kuomba nitumie busara kuzuia jazba na maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa niliongea na wanafunzi na niliwasihi watulie na nilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na kwa bahati nzuri nilimpata Mkuu wa Mkoa na kumweleza juu ya kifo hicho na kile ambacho wanafunzi wanakusudia kufanya kuandamana kwenda ofisini kwake. Nilimuomba afike ili aweze kutuliza hali hile na pia atoe kauli juu ya tukio hilo baya la kuhuzunisha kwani ikizingatiwa kuwa ni zaidi ya mara moja matendo kama haya yamekuwa yakitokea na hakuna hatua zozote zimekuwa zikichukuliwa kuwahakikishia Wanafunzi Usalama wao na mali zao.

Mkuu wa Mkoa pamoja na mimi kumpa taarifa mapema aliahidi kufika mapema jambo ambalo halikufanyika na wanafunzi walianza kuwa wakali na nilifanya jitihada na hekima za hali ya juu kuvuta subira za wanafunzi hao ili Mkuu wa Mkoa afike . Baada ya Mkuu wa Mkoa kufika Makamu wa Chuo aliniomba niwaandae wanafunzi kumsikiliza Mkuu wa Mkoa na yeye alikwenda kumchukua Mkuu wa Mkoa na kumpa mukutasari wa tukio zima na hali halisi ya kilichokuwa kinaendelea na kimsingi Mkuu wa Mkoa alipofika Wanafunzi walitaka apande juu kuongea mahali ambako tulitumia kama jukwaa kwa maongezi wakati wote lakini badala yake mambo yafuatayo yalianza kutokea 

1)  Mkuu wa Mkoa alikataa na kunitaka nishuke chini mahali alipokuwa yeye na timu yake ya ulinzi na usalama Mkoa kwa kweli nilitii na nilipotaka kuongea nae alinidharau na kuniambia hawezi kuongea na wanafunzi wahuni wasiokuwa na nidhamu maneno ambayo yaliwatia wanafunzi hasira zaidi na nilimsihi na kumuomba Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa (RSO) kumshawishi Mkuu wa Mkoa kukubali kuongea nao kwani hali ilivyokuwa ni dhahiri kwamba wanafunzi wale walikuwa na jazba ya hali ya juu na hivyo hekima na unyenyekevu ndio ilikuwa njia pekee ya kutuliza hali hile. 

2)  Mkuu wa Mkoa alitoa masharti kwamba asingeweza kuongea nao bila kipaza sauti na wanafunzi wote waende jengo lililokuwa karibu na Utawala na wakisha kaa atakuja kuongea nao jambo ambalo wanafunzi waligoma kwa imani kwamba jengo hilo lisengeweza kuchukua wanafunzi wengi na mimi niliaga naondoka kwenda msibani na wanafunzi waligoma nisiondoke mpaka watakapo sikilizwa na kwa kweli nilitii maombi baada ya kunizuia na kukaa mbele ya gari yangu.

3)  Tulipokwenda eneo la kukutania na mara hii ilikuwa ni nje jirani ya jengo la utawala wanafunzi walikusanyika wakimsubiri Mkuu wa Mkoa na kabla hajafika nilitwa na yeye mwenyewe ili tuweke msimamo wa pamoja kama viongozi lakini badala yake alitumia Polisi kunitisha na kuhaidi kuwa nitamtambua kuwa yeye ni Serikali ,tulitofautiana tena nilipokataa hofu hiyo na ghafla tuliamua kwenda eneo la kuongea na wanafunzi na ndipo yafuatyo yalitokea “


Mkuu wa Mkoa wakati anaanza kuongea alianza kusema maneno yafuatayo “ Mnaona hiki Kifua na huu mwili wangu , na hapo ndipo hali ilipochafuka na kuamsha vurugu kubwa kutoka kwa Wanafunzi waliokerwa na kauli yake na Polisi wa walimchukua na tafrani kati ya Polisi na Wanafunzi ikapamba moto hali iliyosababisha mabomu ya machozi kulipuliwa kwa wingi kila kona ya chuo na kila mtu kuanza kukimbia kuangalia usalama wake nikiwemo mimi .
Nimesikiliza Mkutano wake na Waandishi wa Habari na leo nimesoma nakusikiliza vyombo mbali mbali vya habari kwamba ninatafutwa na Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa , nimeshangaa sana japo sio kumshangaa Mkuu huyu wa Mkoa kwani ufahamu na uwezo wake naujua ulivyo katika kufikiri na kutatua mambo ya msingi na muhimu , kwa jinsi nilivyomsikia na kumuona alivyokuwa anashughulikia tatizo lile lililotukutanisha jana pale Chuoni , kwa kweli nilishangazwa sana na kuogopa kama hekima ya Mkiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa angeweza kushughulikia tatizo lile kwa namna ile ya Kiburi , Dharau na Majivuno ambayo hakika ilikuwa ni chanzo cha wanafunzi kukataa kumsikiliza na ndipo alipoamua kuondoka huku zomea zomea ikiendelea kushamiri vizuri . Mabomu yalianza kupigwa , wanafunzi walipigwa na kunyang’anywa pesa , simu , na lap top na vitu mbali mbali ambavyo Polisi walikuwa wanaona vina thamani kwao , nilikuwa ninatazama mambo haya huku roho yangu ikiwa inauma sana kwamba wanaopaswa kulinda usalama wa raia na mali zao ghafla waligeuka kuwa vibaka wa kuumiza raia na kupora mali zao .

Ninawapa pole wanafunzi kwa msiba wa rafiki yao na siku ya jana ilikuwa ni siku ya Serikali kutumia busara kurudisha matumaini kwa wanafunzi wale pamoja na raia , lakini badala yake wafiwa walipotaka kudai haki zao za kulindwa , walipigwa , walidhalilishwa na Chuo chao kufungwa bila sababu ya msingi wala kuzingatia mambo muhimu .

Ifahamike kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha kina wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii, na amri ya mkuu wa mkoa kufunga chuo na kuamuru wanafunzi watawanyike ifikapo saa kumi na mbili jioni , huu ni ukosefu wa upendo , hekima , busara na utu ikizingatiwa kuwa sababu na mchochezi wa vurugu hizi ni Mkuu wa Mkoa kukosa maarifa na hekima.

Nimepokea ujumbe katika simu yangu kutoka kwenye simu yangu ya kiganjani kutoka kwa Mkuu wa Mkoa inayonitishia na kuweka maisha yangu kwenye hali ya hatari na ujumbe huo unasema “ UMERUKA KIHUNZI CHA KWANZA , NITAKUONYESHA KUWA MIMI NI SERIKALI ULIKOJIFICHA NITAKUPATA NA NITAKUPA KESI NINAYOTAKA MIMI “ Mwisho wa kunukuu .

Mwisho, Ninamshukuru kijana aliyerekodi tukio lote kuanzia mwanzo mpaka mwisho na hivi tutanza kusambaza video cd hizo Nchi ili watanzania wajue ukweli na Mh Rais aone utendaji mbovu wa wateule wake na vile nilitake Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria , maadili ,taratibu na kanuni za kazi na sio kuendesha Jeshi kwa matakwa ya kisiasa , kufanya hivi ni kuhatarisha usalama na utulivu wa Nchi yetu . 

“ Che Guavera alisema “ if you tremble indignation at every injustice then you are a comrade of mine “ 

Wanafunzi jipeni moyo bado kitambo kidogo Taifa hili litabadilika .


Godbless J Lema ( MP)

habari na 

No comments:

Post a Comment