Monday, June 17, 2013

KUTOKA BARAZA LA WAKILISHI ZANZIBAR: Waziri Aboud ataka kasoro zilizojitokeza kwenye Muungano zijadiliwe kwenye mchakato wa Katiba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed (kulia), akibadilishana mawazo na Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar leo.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu (kushoto), akibadilishana mawazo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir (katikati) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar leo.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza, akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri, Thuwaiba Edington Kisasi (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir (kulia) katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar leo. (Picha zote na Yussuf Simai - Habari Maelezo, Zanzibar)


Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeeleza kuwa  kasoro zinazojitokeza katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania zinapaswa kuingizwa na kujadiliwa  katika mchakato wa Katiba unaoendelea.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Nassour Juma, aliyetaka kujua vigenzo vya  uteuzi wa Waziri Mkuu unaofanywa na Rais na Zanzibar imetoa Mawaziri Wakuu wangapi tokea kuasisiwa Muungano.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ambayo hadi sasa ndio inayotuongoza haikueleza vigezo vya uteuzi wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania bali imetoa mamlaka ya uteuzi huo kwa Rais, na tangu kuasisiwa kwa Muungano  hadi sasa Zanzibar imetoa  Waziri mkuu mmoja ambae ni Salim Ahmed Salim.

Alifahamisha kuwa tangu kuasisiwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Zanzibar haijawahi kutoa Spika wala Naibu Spika isipokuwa imewahi kutoa Mwenyekiti wa Bunge Zubeir Ali Maulid katika kipindi cha mwaka 2005/2010.

Hata hivyo Waziri Aboud alisema kuwa  nafasi bado ipo ya kuweza kueleza kero  zilizopo ambazo zinaonekana kwamba ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muuungano ya Tanzania.

Alikiri kuwa ipo hati ya makubaliano na maridhiano ya kikatiba kwa nchi  zote mbili zilizokuwa huru na mamlaka yake kamili na pia si kweli kuwa Zanzibar haina wasomi .

Waziri alieleza kuwa kero za Muungano bado zipo na ndio sababu moja wapo ya  kuanzisha mchakato wa katiba ili kuzitafutia ufumbuzi  kero hizo.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema  kuwa wanavyojuwa  ni kua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja kero zilizozopo zinafanywa kwa makusudi. 

No comments:

Post a Comment