Monday, June 17, 2013

NCHIMBI AAPA KUWAKAMATA WAHUSIKA WA MLIPUKO WA BOMU ARUSHA


Siku moja baada ya kutokea kwa mlipuko wa Bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu JOSEPH Parokia ya Olasiti jijini Arusha na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi 58 jeshi la polisi nchini tayari linawashikilia watu Sita wakiwemo raia wanne wa kigeni.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. EMMANUEL NCHIMBI amesema tukio hilo lilitokea wakati wa uzinduzi wa Parokia ya Olasiti huku Balozi wa Vatikani nchini akiwa ni mgeni rasmi ambapo Bomu la kurushwa kwa mkono lilirushwa kuelekea kwenye mkusanyiko wa watu.
Kufuatia hali hiyo kimeundwa kikosi maalum kwaajili ya kufanya uchunguzi huku Serikali ikiahidi kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kuhusika na shambulio hilo linalochafua taswira ya nchi.
Wakati huo huo Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi imewasilisha Bajeti yake kwa mwaka wa Fedha 2013/2014 na kuahidi kuendelea kupambana na uharifu ambapo kambi rasmi ya Upinzani bungeni imetaka kufanyiwa kazi kwa masuala ya uvunjifu wa amani kutokana na matukio yanayoendelea kujitokeza.
Kwa upande wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Msemaji wa kambi hiyo kwa Mambo ya Ndani ya nchi VICENT NYERERE amependekeza msongamano wa wafungwa magerezani upunguzwe kwa kutoa adhabu mbadala na kubadili ratiba za kula na kulala kwa Wafungwa na Mahabusu.

Serikali imewataka watanzania wakiwemo wakazi wa jiji la Arusha kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati vyombo vya dola kwa kushirikiana na raia wema wakiendelea kufanya uchunguzi wa kina juu tukio la mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni mlipuko katika uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.


Wito huo umetolewa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dokta Emmanuel Nchimbi wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembela eneo la tukio na kuwajulia hali majeruhi wa tukio hilo waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini Arusha.



Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo baada ya kuwajulia hali majeruhi hao amesema binafsi tukio hilo limemsikitisha ambapo ameendelea kuwasihi majeruhi, wafiwa pamoja na wakazi wa jiji la Arusha kuendelea kuwa wavumilivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Kufuatia mlipuko huo watu kadhaa wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 60 wamelazwa katika hospitali mbalimbali zilizopo jijini Arusha ambapo baadhi ya majeruhi wameeleza hisia zao kusiana na mlipuko huo huku wakimtaka mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo achukua hatua stahiki dhidi ya tukio hilo.

Aidha Rais Jakaya Kikwete ambaye yupo ziarani nchini Uingereza ametoa pole kwa wale waliopoteza maisha, majeruhi; Uongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo pamoja na wananchi wa jiji la Arusha kwa ujumla Kufuatia mlipuko huo na kusema kwamba amehuzunishwa sana na tukio hilo na kuagiza vyombo vya dola kuharakisha uchuguzi wake.
Tume ya taifa ya uchuguzi NEC imehairisha hadi tarehe 30 mwezi huu uchaguzi wa mdogo wa madiwani katika kata nne za mkoani Arusha.

habari kwa hisani ya http://haazu.blogspt.com

No comments:

Post a Comment