Washukiwa wa
kundi la wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, wamewaua wanafunzi tisa
, katika shambulizi la pili ambalo limewalenga wanafunzi katika siku za
hivi karibuni.
Washambuliaji
wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram,
waliwashambulia kwa risasi wanafunzi hao waliokuwa wamevalia sare za
shule katika shule moja viungani mwa mji wa Maiduguri.
Boko Haram ilikiri kufanya mashambulizi hayo na kusema ilikuwa adhabu kwa vijana kwa kuunga mkono jeshi.
Baadhi ya manusura walisema kuwa ilikuwa hatua dhidi ya kuibuka kwa makundi ya vijana wanaotoa ulinzi kwa raia mjini humo.
Eneo la
Kaskazini mwa Nigeria, liko chini ya sheria ya hali ya hatari huku
serikali ikijaribu kupambana na kundi la Boko Haram pamoja na harakati
za makundi ya kiisilamu.
Mmoja wa walioshuhudia Ibrahim Mohammed alisema alikuwa darasani akifanya mtihani wakati watu hao walipovamia jengo hilo.
"niliona wanafunzi watano, waliokuwa wanafanya mtihani wakiuawa papo hapo.''
''Wanafunzi wengine, waliuawa walipokuwa wanaingia shuleni''
Wafanyakazi wa
hospitalini walithibitisha kuona miili ya watoto tisa wakiwa bado
wamevalia sare zao wakipelekwa katikia chumba cha kuhifadhia maiti
Maiduguri.
Msemaji wa Boko
Haram, aliwaambia waandishi wa habari kuwa shambulizi hilo lilikuwa la
kulipiza kisasi na onyo kwa vijana kwa kusaidiana na jeshi.
Makundi ya vijana wanaotoa ulinzi wamekuwa wakiwakamata washukiwa wa Boko Haram na kuwakabidhi kwa jeshi.
Msemaji wa jeshi alisema kuwa wale waliokabidhiwa kwa polisi watafikishwa mahakamani na kutendewa haki.
No comments:
Post a Comment