Tuesday, August 27, 2013

Baraza la Katiba Mambo ya Nje lapendekeza Urai wa nchi mbili


Na Magreth Kinabo na Eleuteri Mangi – Maelezo
BARAZA la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa limependekeza kuwa   Watanzania waliopo nje ya nchi wasifutiwe uraia wa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe  wakati alipokuwa akichangia suala la uraia katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba kupitia baraza hilo kwenye ukumbi wa  mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dares Salaam.

“Raia  wa Tanzania aliyeko  nje ya nchi  na kuomba uraia wa nchi hiyo kwa sababu  yoyote ile  iwe  ya elimu, afya au  ajira asifutiwe uraia wa Tanzania,” alisema Waziri Membe.

Waziri Membe, aliongeza kuwa Watanzania waliopo nje ya nchi ambao ni waaminifu  hawawezi kupata ajira rasmi ‘white collar job’ hivyo  kishia kufanya kazi zisizo rasmi.

Alifanunua kwa Watanzania walioamua ‘kujilipua’ yaani kuukana uraia wamepata kazi nzuri lakini hawasaidii taifa lao la asili.
Kauli hiyo ya Waziri Membe iliungwa mkono wa baadhi ya mabalozi waliotumikia Tanzania katika nchi mbalimbali wakati mjadala huku wakitaka suala liwekewe utaratibu ili kuokoa nguvu kazi ya taifa na wataalamu  mbalimbali walioko nje ya nchi.

Miongoni mwa mabalozi waliounga mkono ni Balozi Martin Lumbanga ambaye alisema “Suala la uraia wa nchi mbili ninaliunga mkono kwa kuwa lina faida nyingi kuliko hasara,”alisema.

Balozi  Paul  Rupia  alisema ni wakati umefika  kwa Watanzania kuwa  na uraia wa nchi mbili, hivyo suala hilo  lisiogopwe bali liwekewe utaratibu unaofaa.

“Ni  vema tuliwekee utaratibu ili tuendelee kuwa na watu wetu bila kuwapoteza,”alisema Balozi Rupia.

Kwa mujibu wa Waziri Membe alisema  hivi sasa Watanzania waliopo nje ya nchi ni milioni tatu  kati ya Watanzania zaidi milioni 44.

Baraza hilo lilihudhuriwa na  mabalozi hao, makatibu wakuu kiongozi wastaafu, na watumishi mbalimbali wa wizara hiyo ambapo aliazimia suala hilo liingizwe kwenye mchakato wa  rasimu ya Katiba.

No comments:

Post a Comment