Friday, August 23, 2013

Wakala wa Usafiri wa Haraka yaelezea utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi wa Mfumo na Maendeleo kutoka Wakala wa Usafiri wa Haraka Mhandisi John Shauri akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini leo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Frank Mvungi-MAELEZO)

TAARIFA YA MAWASILIANO YA SERIKALI  KWA UMMA KUHUSU  MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM


(DAR RAPID TRANSIT – DART)

 

1.0 UTANGULIZI  


1.1 UANZISHWAJI WA WAKALA


Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit - DART) ulianzishwa kupitia Notisi ya Serikali, Namba 120 ya tarehe 25 Mei 2007 na kuzinduliwa rasmi tarehe 16 Juni 2008 ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Mfumo wa Usafiri wa Haraka. Wakala una malengo makuu matatu ya utekelezaji;

(i)       Kusimamia utekelezaji na uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam;

(ii)       Kuweka mpangilio makini wa matumizi ya barabara kuu na ndogo kwa  watumiaji wote ili kupunguza msongamano; na

(iii)     Kuhakikisha kuwepo kwa menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo   Haraka yenye kuleta tija na ufanisi.

1.2 DIRA YA MFUMO WA DART


Kuwa na usafiri bora wa umma wenye gharama nafuu unaotumia mabasi ya ujazo mkubwa yaendayo kwenye njia maalum uzingatiao mazingira na kwenda kwa wakati.


kutoa huduma bora na nafuu Jijini Dar es Salaam na kuleta ukuaji wa uchumi endelevu kwa wananchi na kuwa kichocheo baina ya sekta ya umma na sekta binafsi katika nyanja ya usafirishaji wa umma mijini.

2.0 MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA


Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ulibuniwa mwaka 2002 chini ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Utekelezaji wake ulianza kwa kazi ya Usanifu wa mradi ambao ulifanyika kwa hatua kuu mbili.

2.1 USANIFU WA MRADI


Usanifu wa Ujumla (mwaka 2005) uliofanikisha kupatikana kwa michoro ya awali, makadirio ya gharama na mchanganuo wa kibiashara (business plan) pamoja na jinsi ambavyo mradi ungeweza kutekelezwa kwa awamu sita kama ifuatav


AWAMU

BARABARA ZITAKAZOHUSIKA

UREFU (KM)

1

Morogoro, Kawawa (kaskazini), Msimbazi, Kivukoni

20.9

2

Kilwa, Kawawa (kusini)

19.3

3

Nyerere, Uhuru, Bi Titi, Azikiwe

23.6

4

Bagamoyo na Barabara ya Sam Nujoma

16.1

5

Mandela, Barabara mpya

22.8

6

Old Bagamoyo, na barabara mpya mbili

27.6

 

JUMLA

130.3

 2.2 USANIFU WA KINA


Usanifu wa kina wa miundombinu ya awamu ya kwanza ambayo inajumuisha pamoja na njia maalum za mabasi, vituo vikuu (terminals) 5, vituo vya mabasi 29 na vituo vya maegesho (Bus depot) 2 ulikamilika mwaka 2007. Mradi pia utahusisha ujenzi wa njia maalumu za waenda kwa miguu na baiskeli na vivutio vya mji kama vile bustani za mapumziko (Kwa ushirikiano na sekta binafsi).Kufuatia usanifu huo, Halmashauri ya Jiji iliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzisha Wakala ambao utatekeleza mradi wa DART na masuala mengine ya usafiri hususan usafiri wa umma.

2.3  JUKUMU LA WAKALA


 Jukumu kuu la Wakala katika kipindi hiki ni utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit – DART). Mradi huu unalenga katika kuongeza tija na ufanisi katika kuchochea kasi ya maendeleo katika Jiji la Dar es salaam na taifa zima kwa ujumla hasa tukizingatia zaidi ya 80% ya pato la ndani la Taifa linachangiwa na Jiji la Dar es salaam.
 

Sheria na taratibu zinazoongoza utekelezaji wa mradi huu, ni pamoja na makubaliano (Financing Agreement) kati ya serikali na Benki ya Dunia, Sheria ya Ardhi na Mwongozo (Resettlement Action Plan) kuhusu ulipaji wa fidia kwa mali na watu watakaoathiriwa na ujenzi wa miundombinu ya mradi.  Pia sheria iliyoanzisha SUMATRA inazingatiwa kikamilifu katika maandalizi ya utoaji huduma.

2.4 GHARAMA ZA MRADI


Mradi unagharimiwa na fedha toka Benki ya Dunia (Dola za Kimarekani  325.37 milioni na Serikali ya Tanzania imechangia shilingi 23.5 Bilioni kwa ajili ya kugharimia ulipaji fidia mali zilizoathiriwa na miundombinu ya mradi. Sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Dola za Kimarekani 100 milioni kwa ajili ya kuwekeza kwenye ununuzi wa mabasi na mfumo wa kisasa wa ukusanyaji nauli na utunzaji wa fedha zinazotokana na mfumo.

Mchango wa Serikali Kuu pia inachangia gharama za Mishahara,Fedha za uendeshaji wa Wakala za Matumizi ya Kawaida na vifaa vya uendeshaji na usimamizi wa mradi.

Utekelezaji wa mradi huu unashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wakazi wa Jiji la Dar es salaam pamoja na vitongoji vyake.  Aidha, wadau wakuu ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ujenzi,Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na  Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika Jiji la Dar es Salaam, Benki ya Dunia, na Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA).    

 Katika Kipindi  cha utekelezaji cha Mwaka 2010/2011 na 2011/12 Ujenzi wa miundombinu awamu ya kwanza ulianza kutekelezwa kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Barabara (TANROADS) kufuatia uzinduzi rasmi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 10 Agosti 2010 katika eneo la Kituo cha Mabasi cha Kivukoni.

Katika kipindi hicho, Makandarasi walioanza shughuli za ujenzi ni pamoja na Beijing Construction Engineering Company anayejenga Kituo cha Kivukoni, Vituo Mlisho. Mkandarasi Mkuu wa ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya njia  maalum za DART  kampuni ya Strabag ya Ujerumani ilipatikana katika kipindi hiki cha utekelezaji cha Mwaka 2011/2012.

2.5 UTEKELEZAJI wa shughuli zilizopangwa na gharama ya fedha kwa mwaka 2012/13


Shughuli kubwa katika kipindi hiki ni ujenzi wa miundombinu ya mfumo awamu ya 1 unaendelea kwenye barabara ya Morogoro kuanzia Kimara mpaka mjini kati na Kivukoni ambao unatarajia kukamilika mwaka 2014. Ujenzi wa Barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni mpaka Morocco na Mtaa wa Msimbazi eneo la FIRE mpaka Gerezani Kota ujenzi utakamilika mwaka 2015.

Katika awamu hii ya kwanza, mtandao wa barabara za DART unahusisha njia kuu kuanzia Kituo Kikuu cha Kivukoni, karibu na kivuko cha kigamboni na kupitia Kivukoni Front hadi barabara ya Morogoro, na kuishia katika Kituo Kikuu cha Kimara, kwa kupitia Kituo Kikuu cha Ubungo karibu na makutano  ya barabara ya  Nelson Mandela / Sam Nujoma. Aidha, awamu hii ya kwanza inajumuisha ujenzi wa matawi mawili ya Barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Kituo Kikuu cha Morocco na Mtaa wa Msimbazi ikiishia Kituo Kikuu cha Kariakoo.

2.6   Usimamizi wa Ujenzi wa Miundombinu 


Utekelezaji wa Ujenzi wa Miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mabasi ya Haraka (DART) Dar es Salaam –, unasimamiwa na kampuni ya ushauri kutoka nchini Australia iitwayo SMEC International Pty. Mkataba wa usimamizi wa utekelezaji wa mradi huu, kati ya kampuni hiyo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulitiwa saini tarehe 16 Julai 2009. Mkataba wa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya mradi huu utagharimu shilingi bilioni 2.5.

3.0     UJENZI WA MIUNDOMBINU


Ujenzi wa Miundombinu ya DART Awamu ya Kwanza unajumuisha miundombinu ifuatayo:

 3.3.1  Barabara


  Ujenzi wa barabara yenye urefu wa jumla ya kilomita 20.9 ambao unajumuisha barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni, Barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Kariakoo- Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Morocco.Ujenzi unahusisha njia maalumu za mabasi  ya DART ambazo zinajengwa katikati ya barabara kwa zege (cement concrete). Barabara hizi zitakuwa na njia moja kwa kila mwelekeo zenye upana wa wastani wa mita 3.5 kutegemeana na upana toka sehemu moja hadi nyingine. Katika sehemu za vituo vya mabasi, kutakuwa na njia mbili kila mwelekeo kuwezesha basi moja kupita basi jingine.

 Aidha, kunajengwa njia mbili kwa kila mwelekeo kwa ajili ya magari mchanganyiko.Barabara za magari mchanganyiko zinajengwa kwa lami kama kawaida. Aidha Sehemu ya kutoka Kibo hadi Kimara inajengwa njia moja kwa magari mchanganyiko kwa kila mwelekeo. Mtaa wa Msimbazi, utajengwa barabara moja moja ya mabasi na magari mchanganyiko kwa kila mwelekeo.

 Sehemu ya barabara ya Morogoro kutoka makutano ya barabara ya Bibi Titi na  barabara ya Sokoine, kunajengwa njia maalumu za mabasi moja kwa kila mwelekeo pamoja na njia za waendao kwa miguu tu. Magari mchanganyiko hayatakuwa na njia ya kupita katika kipande hiki.Vizuizi vitawekwa ili kutenganisha njia ya mabasi na ile ya waendao kwa miguu.Kivukoni Front, kumepangwa kujengwa barabara moja ya magari mchanganyiko kwa mwelekeo mmoja tu. Tathmini inafanywa kuangalia uwezekano wa kuongeza njia ya pili kwa mwelekeo mwingine.

3.3.2   Vituo vidogo


 Vituo vidogo vya abiria (Bus Stations) vinajengwa katikati ya barabara. Awali, ilipangwa kujengwa  vituo vidogo 29; lakini kutokana na sababu za kiufundi na uendeshaji, vituo viwili vimeondolewa yaani kituo cha Chai Bora karibu na Tanesco Ubungo na kituo cha Kempiski mbele ya hoteli ya Kilimanjaro. Vituo vitakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 65 kwa saa kwa kila mwelekeo.

3.3.3 Vituo Mlisho (Feeder Stations)


 Kutakuwa na Vituo Mlisho (Feeder Stations) sita (6) katika maeneo ya Shekilango, Urafiki, Kinondoni A,Mwinjuma, Magomeni na Fire.Vituo hivi ndiko mabasi madogo yatakapokuwa yakishusha na kupakia abiria waingiao na kutoka katika mfumo wa mabasi makubwa wa DART aidha wakitokea au kuelekea maeneo ambayo mfumo huo wa mabasi makubwa bado haujafika.

3.3.4   Vituo Vikuu (Terminals)

 Kutakuwa na Vituo Vikuu (Terminals) vitano (5) katika maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo, na Kivukoni.Vituo hivi ndiko mabasi yatakapokuwa yanaanzia na kumalizia safari. Vitakuwa mahsusi kwa ajili ya kubadilishana abiria kati ya njia kuu na njia mlisho (feeder roads). Hivi vitakuwa vikubwa na vya kisasa ili kutoa nafasi ya kuweza kuanzishwa kwa huduma za ziada kwenye vituo hivyo na kuruhusu aina nyingine za huduma za usafiri nje ya vituo.

3.3.5   Karakana ya Mabasi (Depot)


 Kutakuwa na karakana mbili (2) katika maeneo ya Ubungo na Jangwani.Mabasi yatasafishwa na kukarabatiwa kwenye karakana hizo. Karakana zitakuwa za kisasa zitakazotoa huduma ya kutosha kwa mabasi kama ukaguzi, usafishaji na ukarabati na sehemu ya kuegeshea mpaka siku ya pili.

3.3.6 Madaraja na Njia za waenda kwa Miguu


 Ujenzi utahusisha njia maalumu za waenda kwa miguu na watumia baiskeli. Aidha kutakuwa na madaraja maalum ya waenda kwa miguu kwa kuvuka toka Vituo mlisho kwenda vituo vya mabasi ya BRT. Madaraja hayo yanajengwa katika vituo vikuu katika maeneo ya Kimara, Ubungo na Morocco.

3.3.7   Miundombinu mingine

  Daraja la Msimbazi eneo la Jangwani linapanuliwa sambamba na ongezeko la njia maalumu za mabasi, baiskeli na waendao kwa miguu. Aidha, upanuzi huo unajumuisha ujenzi wa vyuma vya kuzuia ajali, vya kuongoza magari na njia za waendao kwa miguu. Njia ya waendao kwa miguu iliyopo sasa na sehemu ya ukingo wa barabara vitaondolewa ili kutoa nafasi ya ujenzi wa njia mpya.

Utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya awamu ya kwanza ya mradi unaendelea kwa mgawanyo wa vipengele (Work packages) saba (7) vya mikataba.  Usimamizi wa ujenzi wa awamu ya kwanza upo mikononi mwa TANROADS Makao Mkuu kwa mujibu wa makubaliano (Memorundum of Understanding-MOU) na Wakala wa  DART ya tarehe 16 Juni 2008).

3.3.8 Hali halisi ya ujenzi

Kwa ujumla ujenzi unaendelea vizuri katika maeneo mengi katika awamu hii ya kwanza. Mathalani tukiangalia twakimu za ujenzi kwa mradi mzima ni zaidi ya asilimia 30 hii ikiwa ni pamoja na usanifu wa michoro na ujenzi wa miundombinu ambao unahusisha ujenzi wa barabara za magari yaendayo haraka, watembea kwa miguu, vivuko, waendesha baiskeli, karakana za mabasi maeneo ya Jangwani na Ubungo na vituo vya mabasi. Mpango wa awali, malengo ni asilimia 50 lakini kutokana na changamoto za ujenzi malengo haya hayakuweza kufikiwa. Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na kuchelewa kupatikana kwa  maeneo ya ujenzi- baadhi ya wafidiwa waligoma na kufungua kesi mahakamani.

4.0     MPANGILIO WA UTOAJI HUDUMA


Utoaji huduma kwenye mfumo wa DART unahusisha zaidi Sekta binafsi. Sekta binafsi inatarajia kuwekeza kiasi cha Dolla za Kimarekani 100  milioni kwa ajili ya  ununuzi wa mabasi, na mfumo wa ukusanyaji wa nauli na utunzaji wa fedha ambazo pia zinatakiwa  kuwa tayari mfumo  unapoanza kazi. Yafuatayo yamefanyika kuhakikisha malengo ya utoaji huduma yanafanikiwa.

 

 Makabrasha zabuni za ununuzi wa mabasi, uwekezaji kwenye mfumo wa ukusanyaji nauli na utunzaji wa fedha zinafanyiwa mapitio ili zilingane na uhalisia kitakwimu na kiuendeshaji kutokana na muda mwingi kupita tangu ziandaliwe. Kazi ya mapitio ya makabrasha ya zabuni inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2013.

 

 Wakala wa DART pia umefanikiwa kumpata Mshauri Mwelekezi Mkuu (Chief Technical Advisor) ambaye atasaidia wakala kufanikisha azma yake ya kukamilisha utekelezaji wa shughuli za ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa watoa huduma katika mfumo wa DART wanapatikana katika muda uliopangwa. Wakala unaendelea na  mchakato wa kumpata mtaalam (Trasaction Advisor) atakayeongoza mchakato wa zabuni kazi ambayo imepangwa ianze mwezi Oktoba 2013. Aidha kabla ya kuanza machakato wa zabuni za watoa huduma katika mfumo..

5.0     SHUGHULI NYINGINE KUFANIKISHA MRADI

5.1     Usimamizi, Uratibu Na Ushirikishwaji Wadau


Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu -  Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa  ziliundwa  Kamati za kusaidia kuongeza kasi ya utekelezaji na  usimamizi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Kamati zilizoundwa ni pamoja na Kamati ya Usimamizi inayoongozwa na Meya wa Jiji, Kamati ya Ufundi na Kamati ya Uratibu. Kamati hizi kwa kiasi kikubwa zimesaidia sana kusukuma kasi ya utekelezaji wa Mradi na kutoa msukumo mkubwa katika kutatua changamoto zilizojitokeza.

Aidha  Bodi ya Ushauri ya Wizara (Ministerial Advisory Board) ilizinduliwa tarehe 19 Julai, 2013. Kuzinduliwa kwa Bodi hii kutaendelea kuimarisha usimamizi na uratibu wa mradi.

5.2 Uandaaji Rasimu ya Mwongozo wa Sera ya kuwahusisha wamiliki wa Daladala katika mfumo wa DART


  Katika utekelezaji wa Mradi wa mabasi Yaendayo Haraka awamu ya kwanza jumla ya daladala 1,600 zitahamishwa sehemu nyingine kupisha utekelezaji wa mradi wa mabasi Yendayo Haraka Katika Jiji la Dar es Salaam.Wakala hivi sasa kwa kushirikiana na wadau unandaa rasimu ya mwongozo wa sera ya ushirikishaji wamilki wa Daladala ‘Daladala Transition Policy Framework’’. Aidha Wakala unandaa Mkutano maalumu na wamilki wote wa daladala ili kuendelea kuwahamasisha wajiunge katika Makampuni na baadaye kununua hisa katika uendeshaji wa mabasi yaendayo haraka.

5.3     Ulipaji Fidia


 Ulipaji wa fidia ulianza mwaka 2007 na umefikia hatua za mwisho. Maeneo matatu yaliyokuwa yamebaki yamekamilishwa katika kipindi hiki cha ujenzi.

·        Kituo Kikuu cha mabasi  cha Ubungo:

Zoezi la ulipaji wa fidia katika Kituo Kikuu cha mabasi  cha Ubungo limekamilika. Hadi kufikia Juni 2013 ya wafanyabishara  wote 230 sawa na asilimia 100 walikuwa wamelipwa fidia zao  na  kuhama kupisha ujenzi wa miundombinu ya mfumo DART.

 Magomeni – Bondeni:

Kwa upande wa fidia ya Magomeni – Bondeni wakazi wote 42 waliokuwa wanadai fidia wamelipwa na kupisha uhamishaji wa nguzo za umeme na kazi ya uhamishaji imekamilika.

·        Kariakoo Gerezani:

Kwa upande wa waliokuwa wakazi wa Kariakoo Gerezani – Kota Jumla ya wakazi 81 kati ya 106 wamekwisha chukua fidia zao. Bado kuna baadhi ya waliokuwa wakazi wa eneo la Kariakoo Gerezani ambao bado wanaoendelea na shauri dhidi ya Wakala wa Majengo (TBA).

5.4     Usanifu wa Awamu ya 2 Na 3:


Kampuni ya Ushauri ya M/S Kyong Dong Engineering Co. LTD ya Korea iliyosaini mkataba tarehe 25 Februari 2011 kwa ajili ya kusanifu Miundombinu ya DART awamu ya Pili na  ya Tatu kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2013, baada ya kulazimika kuongezewa muda kutokana na changamoto zinaojitokeza. Changamoto kuu kwenye usanifu wa kina hususan ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa vituo vikuu na Maegesho.

6.0     CHANGAMOTO


 Changamoto kuu ya mradi huu kwa sasa ni:

·        Upatikanaji wa fedha za kulipa fidia kwa wakati.

·        Upatikanaji wa maeneo ya ujenzi.

·        Uondoaji wa vikwazo vinavyojitokeza wakati wa ujenzi

·        Kesi zisizoisha kuhusiana na eneo la Gerezani, waliokuwa wakazi wameendelea kufungua kesi ambazo hazina msingi.

·        Kuwawezesha wamiliki wa Daladala wauelewe mfumo na kujipanga. Juhudi za kuwaandaa hazijazaleta mafanikio yanayokusudiwa kutokana na mtazamo wa kunyang’anywa biashara.

·        Ufinyu wa Bajeti.

7.0     KAZI ZILIZOPENDEKEZWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2013/14


 Serikali imejipanga kuhakikisha ujenzi wa miundombinu unakamilika kwa wakati na upatikanaji wa watoa huduma ya mfumo wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Katika Jiji la Dar es Salaam unafanikiwa. Mambo ya msingi yatakayo tekelezwa ni pamoja na:-

·    Kufuatilia  kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa DART  kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara wa Tanzania (TANROADS) ili ujenzi ukamilike kabla ya Julai 2015;

·    Kukamilisha mikataba na manunuzi ya watoa huduma katika mfumo wa DART watakaohusika katika ununuzi wa mabasi, ukusanyaji wa nauli na usimamizi wa fedha mwaka wa Fedha 2013/14;     

·    Kukamilisha usanifu na kuanza ujenzi wa kituo cha Mawasiliano ya Mfumo wa DART;

·    Kufanikisha ufuatiliaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu awamu ya  2 na 3;

·     Kufanikisha ukarabati wa barabara za mlisho (feeder roads), za mfumo wa DART awamu ya kwanza kupitia Halmashauri za Manispaa za Ilala na Kinondoni kabla ya mfumo kuanza  Julai 2015;

·    Kufanya mkutano maalum (Road show) ili kuwatafuta Wawekezaji katika mfumo wa DART;

·    Kuhakikisha Miundombinu ya Mfumo wa DART inayokamilika kujengwa na inayoendelea inalindwa na kutunzwa ipasavyo kabla ya mfumo kuanza;

·    Kubuni na kuweka  Mikakati ya Kutafuta vyanzo vya mapato katika mfumo wa DART kuipunguzia Serikali gharama;

·    Kutoa mafunzo, usimamizi na uendeshaji wa mradi kupitia vikao vya Kamati ya uratibu, Ufundi, Usimamizi na Bodi ya Ushauri ya Wizara na vikao vya wadau mbalimbali katika Mfumo wa DART kwa mujibu wa sheria.

·         Kukamilisha usanifu wa kina kwa Awamu ya pili na ya tatu  ambao unafanywa na kampuni ya Ushauri ya M/S Kyong Dong Engineering Co. LTD ya Korea kufuatia mkataba uliosainiwa tarehe 25 Februari 2011 kwa ajili ya kusanifu Miundombinu ya DART awamu ya Pili na Tatu.

8.0     HITIMISHO


 

Utekelezaji na kukamilika wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni muhimu sana hata hivyo juhudi zaidi za pamoja na kwa kushirikisha Wadau wote zinahitajika. Lengo ni kuhakikisha mfumo DART unaanza kutoa huduma Julai 2015 au mapema zaidi ili kuwaondolea adha ya usafiri wakazi wa Dar es salaam pamoja na kuhakikisha kuwa msongamano wa magari katika barabara zake unapungua au kuondoka kabisa.

Ili kufikia lengo hilo mapema, mradi huu umepewa kipaumbele na Serikali na uko katika Mpango maalumu wa ”Matokeo Makubwa Sasa’’ (Big Result Now) chini ya usimamizi wa kitengo cha Ofisi ya Rais kinachoitwa “President’s Delivery Unit”.

No comments:

Post a Comment