Friday, August 30, 2013

WAZIRI MKUU ATOA SH. MILIONI 10 KUSAIDIA VIJANA 87 WAJITEGEMEE

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kutoa sh. milioni 10 ili kuwasaidia vijana wanaoishi kwenye kijiji cha vijana cha Tulu ambao wameamua kujitegemea kwa uzalishaji kupitia kilimo, matumizi ya misitu na ufugaji.
 
Alitoa ahadi hiyo jana jioni (Alhamisi, Agosti 29, 2013) wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na vijana wa kijiji hicho pamoja na wakazi wa vijiji jirani vya Tumbili na Lufwisi wilayani Sikonge mkoani Tabora.
 
Kijiji cha Vijana cha Tulu ambacho wenyewe wanakiita Pathfinders Green City (Jiji la Watafuta Njia) kilianzishwa Aprili 2013 kikiwa ni msitu mtupu baada ya kupewa ekari 280 kutoka vijiji jirani vya Tumbili na Lufwisi. Kilianzishwa kikiwa na vijana 68 kutoka katika kata zote 17 za Wilaya ya Sikonge. Hivi sasa kijiji kina vijana 87 wakiwamo wasichana 22 na wavulana 65 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24.
 
Akizungumza na vijana na wananchi wa vijiji hivyo, Waziri Mkuu alisema atawapatia seti moja ya luninga ili waweze kupata taarifa za matukio mbalimbali ya kitaifa na duniani. Alisema wanahitaji pia deck ili wakipata programu za mafunzo za kwenye CD au DVD, iwasadie kuangalia. Aliahidi kuwapatia bajaj moja ili iwasaidie wakati wa dharura waweze kufika makao makuu ya wilaya ambako ni umbali wa kilometa saba kutoka kijijini hapo.
 
“Katika muda wa miezi mitatu ambayo mmekaa hapa kazi mliyofanya ni kubwa. Siku zote mwanzo ni mgumu lakini nimefarijika kwa sababu ninyi mmethubutu. Mmetumia nguvu zenu kubadilisha mazingira ya mahali mlipo. Haya ndiyo maisha plus yenyewe... maisha plus ya uhalisia na siyo yale ya kwenye televisheni,” alisema huku akishangiliwa.
 
“Nimeona bustani, mabanda ya nyuki, mradi wa kufyatua matofali na Mkuu wa Mkoa (Bibi. Fatma Mwassa) amesema anataka mfuge kuku wa nyama na mayai. Mimi nasema, fedha hizi ziwasaidie kufuga kuku lakini wawe wa kienyeji, mfuge kibiashara zaidi mtapata mayai na kuku wa nyama pia mtauza na kupata fedha za kujikimu,” alisema.
 
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Tabora kwa ajili ya mahafali ya chuo cha nyuki yatakayofanyika leo, alienda kukagua kijiji hicho ambacho vijana wake ameamua kufuata mfumo wa ‘maisha plus’. Alisema anatambua changamoto ya uhaba wa maji inayokikabili kijiji hicho na akaahidi kuwatafutia wataalam wa kuchimba visima ili waje kufanya utafiti wa maji katika maeneo jirani kwa vifaa vya kisasa zaidi.
 
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki aliahidi kuwachangia vijana hao sh. milioni tano ili ziwasadie kujiletea maendeleo kwani wamekuwa vijana wa mfano kwa wilaya nyingine na mikoa mingine hapa nchini.
 
Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la kijiji hicho ambalo linatarajia kugharimu sh. milioni 50 hadi kukamilika kwake. Jengo hilo litakuwa na ofisi, ukumbi mdogo wa mikutano na stoo. Pia wanapanga kujenga nyumba 12 za kisasa za kuanzia kwa ajili ya vijana waishio kijijini humo. Hivi sasa vijana wanaishi kwenye nyumba za udongo zilizoezekwa kwa nyasi.
 
Mradi wa kijiji hicho unasimamiwa na Kampuni ya KP Media lakini unafadhiliwa na Halmashauri ya Wilayaya Sikonge ambayo mwaka jana iliwapatia sh. milioni 488 na mwaka huu imepanga kuwapatia sh. milioni 300 ili kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji mali kwa kutumia teknolojia za kisasa.
 
Mapema, Bwana Shamba wa kijiji hicho, Bw. Aggrey Kitundu alimweleza Waziri Mkuu kuwa wamekwishalima ekari 10 kwa ajili ya mbogamboga, alkini wametumia nusu eka kupanda miche ya nyanya 4,640 na miche ya vitunguu 6,500. Wamekwishafyatua matofali 7,542 ya Hydrafoam na matofali mengine 49,558 aina ya funganishi (yenye matundu) yamekwishafyatuliwa. Pia wamejenga mabanda 12 ya kufugia nyuki yenye uwezo kwa kutunza mizinga 1,000 lakini hadi sasa wamekwishatengeza mizinga 600 ya kisasa.
 
Naye Mratibu wa mradi huo wa kijiji cha vijana, Bw. Masoud Kipanya alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu, kijiji cha vijana kinatarajia kuwa na miradi ya ufugaji wa nyuki, uchakataji na usindikaji asali, ufugaji wa kuku wa nyama na mayai na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
 
Miradi mingine ni kilimo cha mbogamboga na matunda kwa kutumia teknolojia ya Green House na umwagiliaji kwa njia ya matone (Drip Irrigation), kilimo cha mazao ya biashara na chakula, mradi wa ujenzi wa nyumba bora na uchongaji wa samani, mradi wa uhifadhi wa mazingira na upandaji miti pamoja na usindikaji nafaka na mazao ya mafuta.

No comments:

Post a Comment