Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Eneo la Maziwa Makuu, Mary Robinson akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya yeye na Bw. Martin Kobler (kulia) ambaye ni Muwakilishi wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO kuwasilisha taarifa zao mbele ya Baraza Kuu la Usalama, katika mkutano wa ndani wa Baraza hilo uliofanyika siku ya jumatano. katika mkutano huo wakuu hao wawili walielezea kuridhishwa kwao na hali ya kijeshi na kisiasa inavyoendelea katika DRC hususani eneo la Mashariki ya nchi hiyo. pamoja na mchakato wa utekelezaji wa Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa kuhusu siasa, amani, usalama na maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa na matarajio kuhusu mazungumzo ya Kampala ( Kampala Talks)
**********
Na Mwandishi Maalam
Baada ya kundi la waasi la M23 kudhibitiwa ipasavyo na Jeshi la Umoja wa Mataifa linalotuliza amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ( MONUSCO) na ambalo ndani yake kuna Brigedi Maalum ( FIB). Jeshi hilo sasa linaelekeza nguvu zake katika kulishughulika kundi jingine la FDLR.
“ Nilipata fursa leo ( jumatano) ya kutoa taarifa mbele ya Baraza Kuu la Usalama kuhusu maendeleo ya kijeshi na kisiasa katika DRC. Kwa upande wa kijeshi, baada ya mapigano yaliyopelekea kudhibitiwa kwa kundi la M23 sasa MONUSCO imeelekeza nguvu zake kwa makundi mengine ya waasi na kwa kuanzia tumeanza na kundi la FDLR ( Democratic forces for the liberation of Rwanda)”
Hiyo ni kauli na Bw. Martin Kobler Mwakilishi Maaluma wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO.
Alikuwa akiwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya yeyé na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika Eneo la Maziwa Makuu, Bi. Mary Robison kumaliza kutoa taarifa zao mbele ya Baraza Kuu la Usalama lililoketi katika mkutano wake wa ndani uliofanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
“Tulianza kulishughulikia kundi la FDLR Novemba 27, na kati ya jana na juzi ( disemba tisa na kumi) kumekuwapo na hatua kubwa zinazofanyika za kusafisha maeneo na mitaa muhimu ambayo inashikiriwa na FDLR. Tunaendelea na kazi hii ambayo ni muhimu sana ya kupambana na makundi yote ya waasi likiwamo hilo la FDLR pamoja na kundi jingine la ADF ( Allied Democratic Forces )ambalo lilo katika eneo la Magharibi sana”. Akasema Bw. Kobler
Akasema kuanzia hiyo novemba 27 na siku za hivi karibu baada ya eneo la Pinga ambalo kwa miaka miwili lilikuwa mikononi mwa FDRL makundi mengine ya waasi wakiwamo wababe wa kivita , hivi sasa na baada ya kukombolewa na njia kufunguliwa kwenda Goma, wananchi sasa wanaweza kusafirisha bidhaa zao na kuwatembelea ndugu zao.
Na kuongeza “ Leo nimeleta ujumbe wa matumaini mbele ya Baraza Kuu la Usalama . Nadhani hali sasa ni tofauti katika DRC na hasa baada ya kumaliza mapigano dhidi ya kundi la M23”.
Akabainisha kwamba maeneo mengi ambayo yamekombolewa MONUSCO imeunda ‘visiwa’ vya uvulivu hali aliyosema imeleta matumaini makubwa kwa wananchi, matumaini ambayo yanaonekana bayana katika macho ya wananchi wa maeneo hayo.
Hata hivyo Bw. Kobler aliyekuwa amefuatana na Bi. Mary Robison amesema bado kuna hati hati lakini kuna fursa pia, fursa ya kwamba baada ya mafanikio haya yote hali haiwezi kurejea tena kule tulikotoka na hatuwezi katika miaka michache ijayo kuanza tena mapigano.
Akafafanua zaidi kwamba nguvu za kijeshi peke yake hazitaweza kulifanya eneo la Mashariki ya Kongo kuwa na amani na utulivu wa kudumu kwa kile alichosema, utashi na ushiriki kutoka kwa wananchi wa eneo hilo ni jambo linalohitajika sana.
Akaeleza zaidi kwamba wananchi wenyewe wanatakiwa kushiriki katika utatuzi wa vyanzo ambavyo vimekuwa vikisababisha mapigano na machafuko ya mara kwa mara akitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na kupigania utajiri mkubwa wa madini ambao nchi hiyo imejaliwa.
“ Kwa kushirikiana na wananchi tunahitaji kufanya kazi pamoja na kuyashughulikia matatizo yote yanayochangia migogoro na machafuko, vinginevyo mafanikio ya kijeshi ambayo yamepatika hivi karibuni yatakuwa hayana maana yoyote na tutarejea kule tulikotoka” akasisitiza.
Aidha Mkuu huyo wa MONUSCO amewambia waandishi hao wa habari kwamba pia amelieleza Baraza Kuu la Usalama kuhusu umuhimu wa mchakato wa waasi kujisalimisha mchako unaohusisha pia upokonyaji wa silaha, usambarishaji wa makundi ya waasi na uunganishwaji wa waasi hao katika jamii ( DDR).
Amesisitiza kwamba mchanto huo wa DDR ni muhimu sana hasa kutoka na dalili za kwamba watu hawaoni tena thamani ya kuendelea na mapigano. “ wanataka kurejea uraiani na kuishi maisha ya kawaida na huu ni muelekeo mzuri na muhimu hatuna budi kuitumia fursa hii na hasa katika kuwapa matumaini mapya vijana”.
Akafafanua zaidi kwa kusema kwa mfano asilimia 70 ya watu katika DRC ni vijana wa umri wa miaka 17 ambao anaamini kwamba wanataka kuwa na maisha bora yenye amani, utulivu na maendeleo.
Akaongeza kuwa baadhi ya wapiganaji wa kundi la FDLR na ambao wengi wao umri wao ni chini ya miaka 30 na wamezaliwa baada ya mauaji ya kimbari wanataka sana kujisalimisha na kwamba katika miezi ya hivi karibu wamekuwa wakijisalimisha bila ya mapigano yoyote.
No comments:
Post a Comment