Pia laua kwa risasi askari na raia
Wananchi waua mgambo wawili
Wananchi waua mgambo wawili
Mkuu wa jeshi la polisi, Ernest Mangu
Habari zilizopatikana jana kutoka katika eneo la tukio na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen zinaeleza kuwa, tukio hilo lilitokea juzi jioni katika msitu wa kijiji cha Kiduni ambako jambazi huyo alikimbilia baada ya kupora fedha kutoka kwenye kituo cha mafuta cha Camel kilichopo kijiji hapo.
Kamanda Zelothe aliwataja askari waliouawa kuwa ni OC-CD wa Wilaya ya Newala, ASP F. 8106 Nurdun Kassim Sif (38) na DC Robert F. 5339 (33) ambao walipigwa risasi sehemu mbalimbali za miili na kufariki dunia papo hapo na kwamba miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Kamanda Zelothe na kusainiwa na na ACP Issa Mnilota, majira ya saa 10:45 juzi jioni, mtu mmoja alifika kituoni hapo akiwa amebeba galoni akihitaji mafuta ya Sh. 2,500.
Taarifa inaeleza kuwa baada ya kupatiwa mafuta hayo, mtu huyo aliingia ndani ya jengo hilo na kuamuru wahudumu wampatie fedha za mauzo ya siku mbili, lakini wahudumu hao walikataa kwa maelezo kuwa hawakuwa na fedha.
Habari zinasema baada ya kupewa majibu hayo, ndipo mtu huyo alipochomoa silaha aliyokuwa ameificha ndani ya koti na kuwalazimisha wampe fedha hizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jambazi huyo inadaiwa kuwa alikuwa na bunduki aina ya SMG ambayo aliitumia kutekeleza mauaji hayo.
Taarifa hiyo ya polisi imeendelea kueleza kuwa, mtu huyo ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi, baada ya kupekua alifanikiwa kupata kiasi cha Sh. 3,299, 180 na kutokomea nazo msituni.
Kufuatia hali hiyo, wahudumu walianza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wananchi ambao walianza kumfukuza umbali wa kilomita nane kabla ya kuingia msituni. Na kwamba akiwa amejificha, jambazi huyo alifanikiwa kumuua mwananchi mmoja kwa kumpiga risasi kichwani na kufariki dunia papo hapo.
Mwananchi huyo alitambulika kwa jina la Hamza Msangaluwa na kuwa wakati anapigwa risasi hiyo pembeni yake walikuwapo OC-CD wa Wilaya ya Newala ASP F. 8106 Nurdun Kassim Sif na DC Robert F. 5339 (33) ambao pia walipigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili na kufariki dunia papo hapo.
Taarifa hiyo ya polisi ilifafanua kuwa askari mwingine, PC Isaya (34) alijeruhiwa vibaya sehemu ya paja na kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Newala.
“Jambazi alifanikiwa kutokomea gizani na kuacha helmeti, koti, raba moja na mzula aliokuwa amevaa,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hizo zinasema kuwa hadi sasa jitihada za kumsaka jambazi huyo zinaendelea na kwamba Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwake.
Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, ameanza kwa kwa changamoto ya kupambana na kasi kubwa ya ujambazi nchini.
IGP Mangu siku ya kwanza baada ya kuapishwa alisema mkatati wake wa kwanza utakuwa ni kupambana na uhalifu. Alirudia kauli hiyo wiki iliyopita alipokutana na vyombo vya habari kujitambulisha akiwa na wasaidizi wake.
WANANCHI WAUA
MGAMBO WAWILI
Katika tukio jingine, watu wawili wanaodaiwa kuwa askari Mgambo wameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kisha kuwachoma moto kwa mafuta ya petroli huku gari lao nalo likiteketea kwa kuchomwa moto.
Mwenzao mmoja alinusurika katia tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Nyancheche wilayani Sengerema, mkoa wa Mwanza kwa kutuhumiwa kujifanya askari polisi kutoka wilaya ya Misungwi.
Tukio hilo limetokea juzi jioni katika kijiji cha Nyancheche, kata ya Kagunga baada ya wananchi kuivamia ofisi ya Afisa Mtendaji wa kata na kuwatoa watuhuhumiwa hao na kuwapiga hadi kufariki papo hapo na kisha kuwamwagia mafuta ya petroli na kuwachoma moto pamoja na gari lao.
Sababu za kuwaua mgambo hao ni kitendo chao cha kwenda kwa mganga mmoja wa kienyeji katika kijiji cha Isole, kata ya Buyagu, wilayani Sengerema na kujitambulisha ni maofisa upelelezi wa Jeshi la Polisi kutoka wilayani Misungwi na kumvisha pingu baada ya kushindwa kuwapatia Sh. 900,000 ili wasimkamate.
Baada ya mazungumzo na mganga huyo wa keinyeji waliyekuwa wanamtuhumu kuwa aliwahi kuwapigia ramli wateja wake na kisha kwenda kufanya mauaji ya watu wasio na hatia, hivyo walikuwa wamekwenda kumkamata ili kujibu tuhuma hizo, vinginevyo alipaswa kuwapa kiasi hicho cha fedha ili wasimkamate.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagunga, Musa Mwiromba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya taarifa juu ya watu hao kuzagaa katika vijiji jirani vinavyopakana, wananchi walijiweka tayari ka ajili ya kuwakamata.
Mwiromba alisema baada ya mgambo hao kufika familia ya mganga huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Bunzari, ilimwita Mwenyekiti wa kijiji cha Isole na alipofika aliwaomba vitambulisho na wakakaidi kutoa na ndipo walipoongozana nao kwenda kituo jirani cha polisi cha Buyagu.
Alisema walipokaribia kituoni walimshusha mwenyekiti wa kijiji na kumwambia kuwa walikuwa wameamua kwenda makao makuu ya wilaya mjini Sengerema kuwasiliana na uongozi wa wilaya ya Sengerema juu ya hatua za kuchukua.
Baada ya kubaini walikuwa hawaeleweki katika maelezo yao, mwenyekiti huyo alitoa taarifa katika kijiji jirani cha Ngoma walikoelekea na kwa kuwatahdharisha wananchi juu ya ujio wa watu hao na ndipo walipoweka mtego, lakini bila mafanikio kwa sababu baada ya kufika kijiji cha hicho walielekea katika kijiji cha Nyancheche.
Baada ya watu hao kufika Nyancheche wakiwa na gari aina ya Mark ll walikwenda nyumbani kwa mwenyeji wao Joseph Mayunga, na wananchi waliwafuata na kuwatia mbaroni.
Inaelezwa kuwa baada ya kuwatia mbaroni waliwapeleka katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa kata, lakini kabla ya kuchukuliwa hatua zozote, wananchi walipiga makelele na kuongezeka na kuanza kuwashambulia kwa marungu na mawe hadi kufa kisha kuwamiminia petroli na kuwachoma moto pamoja na gari lao.
Mwiromba alisema aliyetoroka eneo la tukio kabla ya kuuawa aliwahi kuwa askari mgambo kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Sengerema na kwamba jina lake linahifadhiwa kwa sababu za upelelezi.
Aliwataja kwa jina moja waliouawa kuwa ni Yohana na Kulwa wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 30.
Akiwahutubia wananchi kwenye kijiji cha Nyancheche jana mchana, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilayani Sengerema, aliwaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake wanapowakamata watuhumiwa wawakabidhi katika vyombo husika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment