WABUNGE
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha, Godbless
Lema na Joshua Nassari, wanatarajia kuzindua kampeni za udiwani Kata ya
Sombetini, .
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mgombea wa kata hiyo, Ally
Bananga, alisema kutokana na ratiba ya kampeni ya vyama vya siasa
iliyotolewa na ofisi ndogo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uzinduzi
huo utafanyika katika viwanja vya Mbauda Mnadani.
Bananga alisema maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea vizuri ili
kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa na kuvunja rekodi ya mikutano yote
iliyowahi kufanyika ya chaguzi ndogo za udiwani kwa vyama vyote.
“Makamanda wote wa mkoa, wilaya na kata wanaendelea na maandalizi ya
uzinduzi na mikutano mingine ili tuweze kuichukua Kata ya Sombetini
Februari 9 mwaka huu… tuna imani mkutano huo utakuwa mkubwa kuliko yote
ambayo ilishawahi kufanyika,” alisema.
Hata hivyo, wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanasema uchaguzi huo
unatarajiwa kuwa na mnyukano mkali kati ya mgombea wa CHADEMA, Bananga
na David Leskar wa CCM, mtoto wa aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa kata
hiyo kutokana na historia ya vyama hivyo jijini humo.
NEC ilitangaza kufanyika uchaguzi katika kata 27 nchini ambazo zipo
wazi kutokana na madiwani wake kufariki dunia na wengine kupoteza sifa.
Katika hatua nyingine, Bananga alisema hadi sasa Jeshi la Polisi
mkoani humo bado halijawaita kuwahoji wala kuwakamata waliohusika na
uvamizi wa msafara wake Januari 15, mwaka huu wakati akirejesha fomu za
kuwania nafasi hiyo.
Bananga alisema kundi la vijana wanaowasadiki kuwa ni wafuasi wa CCM,
walivamia gari aina ya Toyota Hillux mali ya katibu mwenezi wa chama
chao wilaya, Emanuel Kombe, na kuwapiga waliokuwamo na kuvunja vioo.
Chanzo;Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment