Tuesday, January 21, 2014

Noah yaua watano wa familia moja

Watu watano wa familia moja wamefariki dunia na wengine wawili kunusurika baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali mkoani Tanga.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:30 mchana katika kitongoji cha Mtakuja, kata ya Misima, wilayani Handeni, kwenye barabara kuu ya kutoka Handeni kuelekea Korogwe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Masawe, gari lililopata ajali hiyo lilikuwa na watu saba wa familia moja, huku wawili wakinusurika katika ajali hiyo.

Kamanda Masawe aliwataja watu waliyokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni, Athumani Yussuph (45), Zahara Chayungo (35), Mwajuma Mzimo (55), Juma Hossein (90) na Zuber Abdulrahman (35) na kwamba majeruhi mmoja ndiye aliyetambuliwa huku mwingine ikisadikiwa aliondoka eneo hilo baada ya ajali.

Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda Masawe alisema ilihusisha gari aina ya Noah yenye namba za usajili T 493 AUH.

Alieleza kuwa gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Miraji Shaban (22) ambaye ni majeruhi ilipofika eneo hilo ilikatika shafti hali iliyosababisha kupoteza muelekeo na kupinduka.

Kamanda Massawe alisema kuwa gari hilo lilikuwa limebeba watu saba wa familia moja na kwamba mmoja wa watu wanaosadikiwa kuwa ni majeruhi ambaye hakufahamika jina alitoweka muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Miili ya marehemu hao ilipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na kuchukuliwa baadaye na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi katika kijiji cha Misima.
Kamanda Masawe alitoa wito kwa madereva kuwa makini wakati wote wawapo barabarani, kwenda mwendo wa kawaida pamoja na kuvifanyia uchunguzi wa mara kwa mara vyombo vya usafiri kabla ya kuanza kuvitumia ili kuepuka majanga kama hayo.

Aidha, aliwataka wasafiri na hata wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapomuona dereva akifanya ukiukwaji wa sheria za barabarani kama vile mwendo kasi, ulevi na kujishughulisha na kitu kingine anapoendesha kama matumizi ya simu za mkononi.

Alisema jamii inategemewa na jeshi hilo katika kufanikisha harakati za kukabiliana na matendo ya uovu zikiwamo ajali za barabarani ambazo huleta ulemavu na kupoteza maisha ya watu kwa kiwango kikubwa.

WAWILI WAFA MBEYA

Wakati huo huo, watu wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine 23 kujeruhiwa vibaya baada ya basi dogo aina ya Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka jijini Mbeya kwenda Tunduma kugongwa na lori la mizigo kwenye mteremko mkali wa mlima Mbalizi katika eneo la Iwambi, nje kidogo ya jiji la Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea jana baada ya lori lililokuwa na tela lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Zambia kufeli breki na kupoteza mwelekeo kabla ya kuliparamia basi hilo namba T 910 BFB ambalo lilikuwa mbele yake likielekea mjini Tunduma kisha magari hayo kupinduka mtaroni.

Kondakta wa Coaster, Michael Julius, alisema walipofika kwenye mteremko huo wa mlima Mbalizi dereva wake aliliona lori likimfuata kwa kasi huku likiwa limepoteza mwelekeo.

Alisema kwa kuwa mbele yao kulikuwa na magari mengine na pembeni kukiwa na korongo, hakuwa na uwezo wa kulikwepa lori hilo na ndipo lilipowagonga kwa nyuma na kusababisha gari lao kuanguka mtaroni na kusababisha vifo na majeruhi.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa lori hilo lilifeli breki na kuanza kuongeza mwendo hali ambayo iliwafanya washtuke na kulifuatilia mpaka lilipoligonga gari lililokuwa mbele yake na kupinduka. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment