Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Watu na
Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari
kuhusu kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kutokana na kupungua kwa kasi
ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali nchini. Kulia ni
Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO,Dar es salaam.
Imeelezwa
kuwa Tanzania inapiga hatua nzuri katika maendeleo ya uchumi kwa nchi
za Afrika Mashariki kutokana na kupungua kwa mfumuko wa bei wa taifa
hali inayoleta unafuu wa maisha kwa mlaji.
Mfumuko
wa bei wa Taifa kwa mwaka 2013 kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi
Desemba umepungua hadi kufikia asilimia 7.9 ikilinganishwa na wastani wa
asilimia 16.0 iliyofikiwa mwaka katika mwaka 2012.
Akitoa
tathmini ya hali ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Desemba 2013 na ule
wa mwaka mzima kuanzia mwezi Januari 2013, Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Watu na Makazi Bw.
Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa mfumuko wa bei nchini
kunatokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma
mbalimbali nchini.
Amesema
mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Desemba umepungua hadi kufikia
asilimia 5.6 kutoka 6.2 za mwezi Novemba 2013 na kubainisha kuwa hali
hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za
vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza
kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na migahawani umepungua hadi
asilimia 6.6 mwezi Desemba 2013 ikilinganishwa na asilimia 7.6 za
mwezi Novemba 2013 huku mfumuko wa bei kwa bidhaa zisizo za vyakula
umepungua hadi asilimia 5.5 kwa mwezi Desema 2013 kutoka aslimia 5.7
za mwezi Novemba 2013.
Bw.
Kwesigabo amefafanua kuwa mwenendo wa bidhaa zote za 224 zinazotumika
kupimia mfumuko wa bei nchini unaonesha kuwa bidhaa za vyakula
zimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mfumuko wa bei.
Akieleza
kuhusu matokeo ya mfumuko wa bei unaopimwa kwa kigezo cha mwezi
amesema takwimu zinaonyesha ongezeko la asilimia 1.3 ikilinganishwa na
ongezeko la asilimia 0.6 kama ilivyokuwa mwezi Novemba huku fahirisi za
bei zikiongezeka hadi kufikia 144.07 mwezi Desemba kutoka 141.23 za
mwezi Novemba na kubainisha kuwa ongezeko hilo limechangiwa na
kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Amesema
baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kuwa
ni pamoja na mchele kwa asilimia 0.2 , vitafunwa kwa asilimia 2.4,
mahindi kwa asilimia 1.4, unga wa mahindi kwa asilimia 1.6, unga wa
muhogo kwa asilimia 3.0 , kuku wa kienyeji kwa asilimia 1.5 na dagaa kwa
asilimia 2.1.
Bidhaa
nyingine ni pamoja na nazi kwa asilimia 11.5, mbogamboga kwa asilimia
5.8, nyanya asilimia 8.3, njegere asilimia 12.6, maharage kwa asilimia
3.7 mihogo kwa asilimia 5.1 na viazi vitamu kwa asilimia 7.2 wakati zile
zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi ni pamoja na
vitambaa vya suruali kwa asilimia 1.2, blauzi asilimia 1.2, huduma za
kufua nguo kwa asilimia 3.6, gesi kwa asilimia 3.4, mafuta ya taa
asilimia 2.1, mkaa asilimia 4.0, mazulia na vifaa vingine vya kufunikia
sakafu kwa asilimia 1.7, mafuta ya dizeli asilimia 1.3, Petroli asilimia
0.2 , huduma za usafi wa nywele pamoja na usafi binafsi kwa asilimia
1.2.
Bw.
Kwesigabo ameongeza kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kwa mwezi
Desemba 2012 na Desemba 2013 mathalani mchele bei imeonyesha kupungua
kwa asilimia 26.6 huku bidhaa nyingine kama mahindi zikipungua kwa
asilimia 9.3, unga wa mahindi 4.4, viazi mviringo 6.3 na karanga kwa
asilimia 9.7.
Aidha
ameeleza kuwa thamani ya shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa
na huduma za jamii kwa mwezi Desemba 2013 umeonyesha kuwa imara kufikia
shilingi 69 na senti 41.
“Napenda
niwahakikishie kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na
mwelekeo imara kwa kipindi chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo
imara kwa kufikia shilingi 69 na senti 41 ” amesema.
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.15 mwezi Desemba kutoka
asilimia 7.36 za mwezi Novemba, huku nchini wa Uganda ukifikia
asilimia 6.7 kwa mwezi Desemba kutoka asilimia 8.7 za mwezi Novemba.
No comments:
Post a Comment