Wednesday, January 22, 2014

Upinzani wataka Assad afikishwe ICC

Viongozi wa baraza la Upinzani nchini Syria

Marekani imesema maelfu ya picha zinazodaiwa kuonyesha ukatili uliofanywa na serikali ya Syria dhidi ya wafungwa, unadhihirisha wazi haja ya utawala wa rais Bashar al Assaad kuondolewa madarakani.

Serikali ya Syria imepuuzilia mbali ripoti hiyo ikiitaja kama chombo kinachotumiwa kumshinikiza rais Assad kujiuzulu.


Awali, Ujumbe wa kundi la upinzani wa serikali ya Syria, uliowasili Switzerland, kwa mazungumzo ya Amani , umesema ni sharti rais Assad na serikali yake wawajibishwe kwa kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya jinai, ICC, kutokana na ushahidi wa kina uliotolewa kwa njia ya picha.

Wanajeshi wa Serikali ya Syria

Katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa upinzani nchini Syria, Badr Jamous, ametoa matamshi hayo baada ya ripoti ya kimataifa inayoonyesha jinsi utawala wa Assad ulivyokiuka haki za kibinadamu kwa kuwatesa , kuwanyima chakula na hata kuwauwa wafungwa wapatao elfu kumi waliokuwa wakizuiwa katika kambi tofauti kutolewa.

"Twatumai watu wa Syria wana Imani nasi. Tuko hapa kwa lengo la kuwa na mapinduzi nchini Syria.Hatutakubali lingine ila kuondolewa madarakani kwa utawala wa Bashar al-Assad na kuwawajibisha wote waliosababisha mauaji ya wasyria hasa wale walioorodheshwa katika picha zilizomo kwenye ripoti iliyotolewa jana. Utawala wa Assad haustahili lengine ila kuwajibishwa kwa kusimamishwa kizimbani ICC.'' Alisema Bwana Badr.

Bwana Badr, amefafanua kuwa upinzani utafanya vyovyote vile kumshinda rais Assad kidiplomasia.

"Tuko hapa kupigana kama vile vita vinavyoendelea nchini Syria, tuko hapa kwa malengo ya kufanikisha mapinduzi, na kupata ushindi wa watu wa Syria." Alisema kiongozi huyo wa Upinzani.

No comments:

Post a Comment