Saturday, March 15, 2014

Dk. Pindi Chana afungua mkutano mkuu wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano, mkoani Morogoro

Mheshimiwa Dk. Pindi Chana Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto akihutubia Wajumbe wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengine ni Nuru Milao Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (wa kwanza kulia), Ummy Jamaly Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa pili kulia) na Charles Elisante Katibu wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Wajumbe wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa katika mkutano huo jana.
Wajumbe wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa katika mkutano huo jana.
Ummy Jamaly, Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Wajumbe wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa siku mbili wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Dk. Pindi Chana (wa tatu kushoto waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara baada ya kuufungua mkutano mkuu wao jana. Wengine ni Nuru Milao, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (wa pili kulia), Tukae Njiku Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Jamaly Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa tatu kulia), Sandra Bisin Mkuu wa Mawasiliano na Ushirikiano kutokt UNICEF na Charles Elisante Katibu wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na mwandishi wetu, Morogoro
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Pindi Chana (Mb), amefungua Mkutano Mkuu wa siku mbili wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mkoani Morogoro ulioanza Machi 11 hadi 12 mwaka huu.
Mkutano huo wa siku mbili unajumuisha wajumbe wa Mabaraza ya watoto kutoka Mikoa mbalimbali nchini.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia  na Watoto  imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na upatikanaji wa haki za watoto kote nchini.  Mojawapo ya jitihada hizi ni pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa ya kushiriki na kushirikishwa katika masuala mbalimbali yanayowahusu. Hivyo basi, uanzishwaji wa Mabaraza ya watoto ni mojawapo ya jitihada za Wizara na wadau mbalimbali wa watoto kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa ya kukutana na kujadili mambo mbalimbali ya utekelezaji wa mikataba ya kitaifa na kimataifa inayohusu  haki na ustawi wao inavyotekelezwa hapa nchini.
Katika miaka ya hivi karibuni, matukio mengi ya unyanyasaji, udhalilishaji na ya ukatili dhidi ya watoto yanajitokeza katika jamii hapa nchini.  Mengine yanasikika na kusomwa katika Vyombo vya Habari, licha ya yale ambayo hayatolewi taarifa. Kwa ujumla matukio haya yote yanaonesha jinsi haki za msingi za watoto zinavyokiukwa.
Hivyo basi, katika kukabiliana na hali hii Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali zinazolenga kuhakikisha kuwa jamii inaelimishwa vya kutosha  ili itambue na kuthamini utu na haki za watoto. Mojawapo  ya jitihada hizo ni:-
Kuandaa Mpango Kazi wa miaka mitatu (2013 – 2016) wa kuzuia na kushughulikia masuala ya ukatili dhidi ya watoto hapa nchini. 
Kuanzisha Mtandao wa Mawasiliano wa Kusaidia Watoto nchini Tanzania (Tanzania Child Helpline). Mtandao huu utatoa fursa kwa watoto na au watu wazima kwa niaba ya watoto kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili kuwezesha waathirika wa ukatili kupata msaada/huduma kwa wakati muafaka na pia kuhakikisha kuwa wahusika wa uhalifu huo wanafikishwa katika mamlaka husika.
Kuwawezesha watoto kupitia wawakilishi wao kushiriki katika mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuratibu uandaaji wa Ajenda ya Watoto ambao imejikita katika maeneo kumi ya uwekezaji kwa watoto hapa nchini ambayo ni kuwekeza katika kuokoa maisha ya watoto na wanawake, kuwekeza kwenye lishe bora, kuwekeza kwenye usafi na udhibiti wa miundombinu ya maji taka katika shule na kwenye huduma za afya, kuwekeza katika kumuendeleza mtoto akiwa bado mdogo, kuwekeza katika elimu bora kwa wote, kuwekeza katika kuzifanya shule kuwa mahala pa usalama, kuwekeza katika kuwalinda watoto wachanga na wasichana dhidi ya VVU, kuwekeza katika kupunguza mimba za utotoni, kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vurugu , udhalilishaji na unyonyaji na mwisho kuwekeza kwa watoto wennye ulemavu.

No comments:

Post a Comment