Friday, March 7, 2014

NDUGAI AWAASA WATANZANIA KUHUSU MUUNGANO

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, amabaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Job Ndugai.
(Na Jovina Bujulu, MAELEZO DODOMA)
Muungano wa Tanzania bara na Zanzibar ni jambo la kujivunia kwa watanzania wote na katika bara la Afrika.

Hayo yamesemwa leo na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Job Ndugai wakati wa mahojiano katika kipindi cha Jambo kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC ONE.

Mh. Ndugai ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kuwa jambo la Muhimu tunalotakiwa kufanya kwa sasa ni kuimarisha na kuboresha Muungano ili tuweze kupiga hatua za kimaendeleo.

“Hatuna budi kuendelea kuuimarisha muungano uliopo ikiwa ni kichocheo cha maendeleo, tumeona mifano kwenye nchi kadha wa kadha zilizo katika muungano mfano nchi Marekani imekuwa mfano bora duniani kimaendeleo hasa kutokana na Muungano uliopo” Alisema Ndugai.

Mh. Ndugai aliongeza kuwa hata Muasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akitukumbusha mara kwa mara kuusimamia muungano wa Tanzania na kuudumisha.

“Muasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akiasa Watanzania wote kuudumisha Muungano wa Tanzania na kuepuka viashiria vyote vinavyoonekana kuvunja muungano, hivyo tushikamane katika kuudumisha”. Alisema Ndugai.

Naye Mjumbe wa Bunge hilo ambaye mjumbe wa secretariati ya marekebisho kanuni za Bunge Maalum Mhesh. Evod Mmanda alisema kwamba miaka 50 ya muungano ni faraja na jambo la kujivunia.

“hatuna budi kwa pamoja kukaa na kuufikiria zaidi Muungano na kutatua changamoto zote zinazojitokeza ili kuudumisha muungano huu na Wasiopenda Muungano  hawana sababu za kutosha” Alisema Mh. Mmanda.

No comments:

Post a Comment