Friday, March 7, 2014

Kizazi kipya kuwasha moto Tamasha la miaka 50 ya Muungano jijini Dar, Machi 8, mwaka huu

Waziri Said Ali Mbarouk

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Said Ali Mbarouk anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la muziki wa kizazi kipya na tenzi, linalotajiwa kufanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es salaam kesho.

Tamasha hilo ni maalum kwa ajili ya  maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar . Kauli mbiu za maadhimisho ya mwaka huu ni Utanzania wetu ni Muungano wetu tuulinde , tuuimarishe na kuudumisha.

Tamasha hilo ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazotarajiwa kufanyika kuelekea kilele cha Miaka 50 ya Muungano tarehe 26.4.2014.

Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano yataambatana na shughuli mbalimbali zitakazowashirikisha wananchi kupitia makangomano, michezo na burudani na kilele chake itakua tarehe 26 Aprili,2014.

 Shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kongamano na utengamano wa kikanda wa Afrika Mashariki, kongamano la Bara la Afrika ,tamasha la muziki wa dansi na taarabu , maonyesho ya Idara na Wizara za Muungano na  mkesha utakaofanyika kuamkia siku ya Muungano.


Aidha maadhimisho haya ya miaka 50 ya Muungano yalizinduliwa Machi 1, 2014 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  kwenye ukumbi wa Salama katika hoteli ya Bwawani Mjini Unguja msisitizo ukiwekwa  kwa wananchi kuendelea kudumisha udugu, amani, umoja na mshikamano.

No comments:

Post a Comment