Michelle Obama alijiunga katika kampeni kwa kutoa ujumbe katika picha yake |
Kampeni ya mtandao kushinikiza kuachiliwa kwa wasichana takriban 200 wa shule nchini Nigeria waliotekwa na wapiganaji wa Boko Haram sasa imeenea kutoka Nigeria, Marekani na Ulaya hadi kusini mashariki mwa Asia, India na hata pia America ya kusini.
Data katika mitandao ya kijamii kwenye vipindi vya BBC zinadhihirisha kwamba alama ya reli au hashtag inayotumika kuonyesha mada inayojadiliwa, kwa mara hii #bringbackourgirls, imetajwa mara milioni 1 na laki 7 katika mtandao wa twitter.
Ni takriban majuma matatu tangu wasichana hao zaidi ya 200 kutekwa nyara na Boko Haram. Hata hivyo ni siku chache tu zilizopita ambapo masaibu yao yamemulikwa katika mitandao ya kijamii.
Kulingana na takwimu zilizoandaliwa na BBC habari zinazohusu kutekwa nyara kwa wasichana hao katika mitandao ya kijamii baada ya kutumiwa alama ya reli #, kabla ya neno 'Bringbackourgirls' au kwa Kiswahili "turejeshee wasichana wetu", habari hizo zinagusiwa katika maeneo tofauti duniani.
Alama hiyo ya reli imesambazwa katika mtandao wa twitter kwa wingi tangu habari hizo zilipochapishwa kwenye mtandao Aprili 23.
Hicho ni kiwango kikubwa sana ikilinganishwa na ilivyokuwa juma moja lililopita ambapo habari hizo zilirudiwa mara 360,000 pekee.
Nini kilichochea kuenea habari kwa kasi katika mitandao ya kijamii?
Pengine tutazame watu mashuhuri ambao wamelivalia njuga swala hili la kutaka wasichana hao kukombolewa, kama vile mkewe Rais wa Marekani Michelle Obama ambaye amechapisha picha yake akiwa na uso wa huzuni na bango mkononi linalotangaza, "Turejesheeni wasichana wetu."
Picha hii imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii mara 40,000.
Picha hii imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii mara 40,000.
Na aliyekuwa wakati mmoja Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alisema kuwa kupata elimu ni haki ya kimsingi ya kibinadamu.
Bi Clinton alisema Serikali ya Nigeria inapaswa kufanya juhudi zaidi kuimarisha usalama wa watu wake.
BBC imeongea na watu mashuhuri zaidi mbali na Hillary Clinton. Miongoni mwao ni mwigizaji maarufu wa filamu kama vile Angelina Jolie aliyekashifu utekaji nyara wa wasichana hao.
Mmoja wa wanamuziki mashuhuri, na mtunzi wa nyimbo, D'Banj, ameambia BBC kuwa kiwango ambacho jamii ya kimataifa imeeleza kusitikishwa na utekaji nyara wa wasichana hao wanafunzi wa Nigeria, kinawasaidia raia wa nchi yake kustahimili huzuni uliowakumba.
Nchi kama vile Uingereza, Ufaransa na Marekani tayari zimewatuma maafisa wake wa usalama kusaidia kuwatafuta wasichana hao.
D'Banj amesema kuwa ahadi za misaada ya kimataifa zinasaidia kutuliza wasiwasi uliokumba raia wa taifa lake. Alisema, 'na sasa baada ya mataifa mengine ya dunia kuingilia, hasa kutoka magharibi, naweza kusema kuwa ingawa kuna hali ya wasiwasi kuhusiana na hali ya wasichana hao, tungali tuna matumaini na kuendelea kuomba kuwa mwenyezi mungu atatusaidia'.
Takwimu kutoka programu ijulikanayo kama Crimson Hexagon inayofuatilia mawasiliano katika mitandao ya kijamii zinaonyesha kuwa habari kuhusiana na kuwataka wasichana hao warejeshwe nyumbani zimerudiwa mara 238, kwa siku mbili zilizopita pekee.
99,000 kati ya habari hizo zilizorudiwa zilitoka Marekani, 52,000 kutoka Nigeria, ishara kwamba Wamarekani waliojiingiza katika mjadala huu wa kutaka wasichana hao kurejeshwa nyumbani wamewapiku Wanigeria wenyewe.
No comments:
Post a Comment