Friday, May 2, 2014

UKAWA waendelea na Kampeni yao Pemba

Kiongozi wa UKAWA Freeman Mbowe, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Baadhi ya viongozi wa UKAWA na wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba Maalim Seif, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Wafuasi na wapenzi wa vyama vya upinzani wakifuatilia mkutano wa UKAWA uliofanyika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba. (Picha na Salmin Said, OMKR) 

Na Hassan Hamad (OMKR)

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umesema utaendelea na kampeni yake ya kutembea nchi nzima kuwafahamisha wananchi juu ya malengo ya umoja huo pamoja na mustakbali wa katiba mpya ya Tanzania.

Akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa viongozi wa Ukawa katika viwanja vya Gombani ya kale Chake Chake Pemba, kiongozi wa Umoja huo Freeman Mbowe amesema umoja huo umekusudia kuwaungunisha watanzania, ili wapate katiba mpya inayotokana na maoni na kuzingatia maslahi yao.

Amefahamisha kuwa umoja huo una dhamira ya kwali, na kwamba kuanzia sasa hawatokuwa tayari kugawanywa kwa misingi udini, ukabila au maeneo.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema kwa kipindi kirefu vyama vya upinzani vimekuwa vikibaguliwa kwa misingi hiyo, na kuahidi kuwa vitendo hivyo sasa vimefikia mwisho.

“Sisi Chadema tumezushiwa propaganda kuwa ni chama cha Kikristo, na wenzetu wa CUF wakaambiwa kuwa ni chama cha Kiislamu. Sasa tumegundua kuwa lengo lao ni kutugawa na sasa hatugawiki tena”, alisisitiza Mbowe.

Kufuatia kusonga mbele kwa UKAWA, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, amesema atavunja na kuunda upya baraza la mawaziri kivuli bungeni ndani ya saa 24, ili kuwashirikisha viongozi wengine wanaounda umoja huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba, amerejea kauli zake kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya serikali, na kwamba ikiwa vitendo hivyo vitaachiwa kuendelea, nchi itashindwa kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia, amesema kitendo cha baadhi wa viongozi wa serikali kwamba iwapo muundo wa serikali tatu utakubaliwa, Zanzibar itakuwa dola ya kiislamu ni chokochoko ambazo hazina ukweli.

Amefahamisha kuwa Waislamu na Wakristo wa Zanzibar wana uhusiano wa muda mrefu na wa Kihistoria ambao hauwezi kutenganishwa, huku akielezea historia ya kanisa la Minara Miwili la Zanzibar ambalo ni miongoni mwa makanisa yenye historia ndefu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Nae Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amewashukuru viongozi wa Ukawa kwa kuonesha umahiri ndani na nje ya bunge, na kuahidi kushirikiana nao katika harakati za kupata katiba mpya inayotokana na mawazo ya wananchi.


Viongozi hao kwa pamoja wamewapongeza wananchi wa Pemba kwa kuonyesha mshikamano katika kupigania haki na maendeleo ya kisiwa hicho, na kwamba ni mahali pazuri pa kujifunza mshikamano.

No comments:

Post a Comment