Friday, May 2, 2014

Wananchi waomba Kituo cha Afya Simambwe kufanya kazi saa 24


WANANCHI wa Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini wameiomba Serikali kusaidia kukiwezesha Kituo cha Afya Simambwe ili kifanye kazi saa 24 ili kuwasaidia muda wote wananchi wanaohudumiwa na kituo hicho hasa wajawazito.

Kauli za ombi hilo zimetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na wananchi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika vijiji vyao alipowatembelea kuangalia changamoto anuai za huduma za kijamii vijijini Kata ya Tembela.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilembo Usafwa, Richard Ngomela alisema licha ya kijiji hicho kuwa takribani umbali wa kilometa tatu na nusu kukifikia kituo cha afya Simambwe wanakitegemea hivyo kuomba wahudumu kufanya kazi saa 24 ili wapate huduma muda wote.

Alisema kitendo cha kituo hicho kufanya kazi mchana pekee kimekuwa kikishindwa kuwasaidia wagonjwa wa usiku na hasa wajawazito jambo ambao limewafanya baadhi yao kuangaika nyakati za husiku kihuduma na wengine kujifungulia nyumbani.

“Kituo hiki kinafanya kazi mchana tu ukienda usiku inakuwa tatizo,” alisema Ngomela. Aliongeza kuwa nyakati za mchana wanapopata mgonjwa kijijini hapo hulazimika kumbeba kwenye sanduku na kutembea naye kwa miguu umbali wa kilometa tatu na nusu kumpeleka kituo cha Simambwe.

Mkazi wa Kata ya Tembela, Jestina Ndele alisema kutokana na Kituo cha Afya Simambwe kutoa huduma zake mchana tu imewapa shida baadhi ya wagonjwa hasa akinamama wajawazito ambao huitaji huduma ya uzazi/kujifungua nyakati za usiku hivyo wengine kulazimika kujifungulia nyumbani.

“…Unajua kujifungua huwezi jua utajifungua muda gani, yaweza kuwa mchana au wakati mwingine kuangukia usiku, sasa inapotokea hali kama hii usiku inatupa shida sana maana tunategemea kituo hicho tu ambacho kwa sasa kinafungwa saa kumi jioni hii imekuwa tatizo kwa wahitaji huduma za afya usiku,” alisema Bi. Ndele.

Mkazi wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Sikujua Jakobo alisema anashangaa kuona kuwa wamefanikiwa kuwa na kituo cha afya jirani lakini viongozi wanashindwa kuweka utaratibu wa kituo hicho kuweza kufanya kazi usiku kwa utaratibu maalumu ili kuwasaidia wanavijiji wanaokitegemea.

Akitolea ufafanuzi ombi hilo la wananchi, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tembela, Elias Kalinga alisema kituo hicho kinashindwa kufanya kazi usiku kwa kuwa mganga na wasaidizi wake wanakaa mbali na kituo hivyo kushindwa kutoa huduma baada ya saa za kazi za kawaida kumalizika.

Alisema licha ya kituo hicho kuwa na baadhi ya nyumba kwa ajili ya makazi ya mganga hazikuwa na hadhi ya kukaa mganga huyo pamoja na wasaidizi wake. “…Zipo nyumba tatu pale za kituo lakini kwa kweli hazina hadhi ya kukaa mtumishi Yule, kwanza madirisha na milango ilikuwa mibovu, hazina vyoo na jingo linguine lilikuwa kama gofu tu, hivyo mganga anakaa mbali yaani Igawilo,” alisema Kalinga.

Hata hivyo alisema kwa sasa utaratibu unafanywa wa kuzikarabati nyumba hizo na tayari baadhi ya wahudumu wa kituo wamekubali kuzitumia hivyo unaandaliwa utaratibu ambao utawawezesha wao kutoa huduma za dharura hata baada ya saa za kazi (usiku) kwa wananchi.

Mganga Mkuu wa Kituo hicho, Salome Mwaipopo alikiri kuwa nyumba zilizopo hazikuwa na mazingira mazuri ya kuishi wafanyakazi kituoni pale na juhudu zimeanza kufanywa ili kukiwezesha kituo hicho kuwasaidia wananchi kimatibabu hata baada ya saa za kazi.

No comments:

Post a Comment