Thursday, July 31, 2014

Congo: Hatuwapi mafunzo ya kijeshi vijana wa Burundi


Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Bujumbura amekanusha madai kuwa vijana wa Burundi wanapewa mafunzo ya kijeshi katika ardhi ya nchi yake.

Balozi Salomon Banamuhere amesema madai yanayotolewa na jumuia za kiraia za Burundi kwamba vijana wa chama tawala nchini humo CNDD-FDD wanapewa mafunzo ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hayana ukweli wowote. Amesisitiza kuwa hakuna kambi za kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa chama tawala cha Burundi katika ardhi ya Congo na ametoa changamoto kwa wanaotoa madai hayo kutoa ushahidi wao.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na jumuiya za kiraia zinaituhumu serikali ya Burundi kuwa imepeleka vijana wa tawi la chama tawala huko Congo kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Vijana hao wanaojulikana kwa jina la Imbonerakure wanafananishwa na wale wa Interahamwe waliohusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. Vijana wa Imbonerakure wanahusishwa na visa vingi vya kushambulia wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Burundi.

No comments:

Post a Comment