Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa
vikishirikiana na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo vimefanikiwa kuvikomboa vijiji 20 vilivyokuwa vikidhibitiwa na
makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha mashariki mwa nchi hiyo. Luteni
Kanali Felix Prosper Basse Msemaji wa Monusco amesema leo kuwa, majeshi
ya Kongo yakiendesha operesheni ya pamoja na Monusco yamefanikiwa
kuvidhibiti vijiji hivyo vilivyoko katika maeneo ya Beni na Libero
katika jimbo la Kivu Kaskazini. Luteni Kanali Basse amesema kuwa,
operesheni hiyo ya pamoja ya kijeshi imefanyika kwa lengo la kukomesha
mauaji, unyanyasaji, ubakaji, uporaji na utumikishaji watoto kwenye
makundi hayo ya waasi. Operesheni katika mji wa Beni ilililenga kundi
la waasi wa Uganda wa ADF/NALU walioko mashariki mwa Kongo.
No comments:
Post a Comment