Friday, June 1, 2012

‘Zanzibar ni salama kwa watalii’



Naibu wa Waziri wa Viwanda na biashara Lazaro Nyalandu
Kufuatia vurugu zilizotokea katika mji wa Zanzibar na baadhi ya makanisa kuchomwa moto na kikundi cha Uamsho, Wizara ya Maliasili na Utalii amewatoa wasiwasi watalii walioko nchini na wanaojiandaa  kutembelea visiwa hivyo wasihofie kwa kuwa ni salama.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, alisema tangu kutokea kwa vurugu hizo, baadhi ya mitandao ya kimataifa imekuwa ikiripoti taarifa za kuwepo kwa hali ya wasiwasi kwa watalii wanaotaka kuja kutembelea visiwa hivyo.


“Kama Waziri mwenye dhamana ya masuala ya utalii, ningependa kuwahakikishia wageni ambao wako nchini na wale ambao wanajiandaa kuja kuwa vurugu hizo zimeshadhibitiwa na serikali na hazikuathiri utalii katika mji huo pamoja na vivutio vya utalii kote nchini,” alisema Nyalandu aliyezungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Balozi Khamisi Kagasheki.


Aidha, alisema amani imerejea katika Mji Mkongwe Zanzibar na hakuna taarifa yoyote ya uharibifu wa maeneo ya vivutio vya utalii vya mji huo wala kuchomwa kwa hoteli au kudhurika kwa raia yoyote wa kigeni.


Alisema siku chache kabla ya matukio ya Zanzibar kulikuwa na matukio manne ya watalii kuporwa katika maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, uporwaji huo ulifanywa na vibaka waliokuwa kwenye pikipiki na kwamba serikali imechukua hatua kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha waliohusika wanatiwa nguvuni ikiwa ni pamoja na kuongeza usalama wa watalii.

No comments:

Post a Comment