Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, ametoa onyo kali kwa maofisa waandikishaji watakaochelewa kufika na kuondoka kabla ya muda katika vituo vya uandikishaji.
Sadiki ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema uandikishwaji jijini humu utaanza kesho na kuhitimishwa Julai 31, mwaka huu.
Alisema takribani wakazi milioni mbili wanatarajiwa kuandikishwa katika BVR na kwa wakazi wenye sifa takribani milioni mbili wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Sadiki, vituo 1,684 vitatumika katika uandikishaji kwa Manispaa za Ilala (396), Temeke (572) na Kinondoni (706).
Alisema Manispaa ya Kinondoni itakuwa na maofisa uandikishaji 1,412 na wa akiba 136, waandishi wasaidizi 706 na wa akiba 136.
Aidha, alisema Manispaa ya Temeke nayo itakuwa na maofisa uandikishaji 1,144, wa akiba 128, waandishi wasaidizi 572 na wa akiba 128.
Alisema Ilala itakuwa na maofisa uandikishaji 792 na wa akiba 144, waandishi wasaidizi 136 na wa akiba 144.
Kwa mujibu wa Sadiki, katika manispaa hizo pia kutakuwapo na ofisa mwandikishaji wa halmashauri, ofisa uchaguzi, maofisa wasaidizi wa majimbo na kata na wataalam wa Tehama.
Sadiki alitoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi na mapema kujiandikisha kwani kinyume chake watapoteza haki yao ya kupiga kura.
Alisisitiza kuwa wasio raia wa Tanzania hawaruhusiwi katika uandikishwaji huo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka maofisa uandikishaji kufika vituoni kwa wakati na kuondoka kwa muda uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kuwaondolea usumbufu wananchi.
Sadik alisema maandalizi yakiwamo mafunzo kwa wahudumu, yalishafanyika kwa manispaa zote.
Akizungumza na NIPASHE juzi, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema vituo vutafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni kila siku.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, kila kituo katika manispaa hizo, kitakuwa na mashine za BVR mbili kwani mashine 8,000 zilizokuwa zikitumika mikoa mingine zinatarajia kuletwa jijini Dar es Salaam na hivyo kuwaondolea hofu ya kukosa kujiandikisha kwa wakazi wake.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wananchi wenye sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu ni 24, 252, 927.
Watu wenye sifa ya kupiga kura katika Jiji la Dar es Salaam ni 2,932,930 kati ya watu 4, 713, 213.
Awali, uandikishaji kwa mfumo wa BVR, jijini Dar es Salaam, ulipangwa kuanza Julai 12, mwaka huu, lakini uliahirishwa kwa ajili ya maandalizi zaidi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment