Tuesday, July 21, 2015

Kova: Tumewanasa walioua polisi Kituo cha Stakishari.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema limewanasa watu wawili na kuua watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi ambao walivamia kituo cha polisi cha Stakishari na kukamata bunduki 16 jijini Dar es Salaam.
Katika uvamizi wa kituo hicho, majambazi hayo yaliwaua Polisi wanne na raia watatu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema, Polisi imewaua majambazi hayo wakati wakipambana.
 
Aidha, alisema jeshi hilo linawashikilia watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliowakamata Julai 17, ikiwa ni siku chache baada ya kuvamia kituo cha polisi na kufanya mauaji hayo.
 
Kamanda Kova aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kabla ya kuwakamata majambazi hayo, kulikuwa ni mapambano makali ya kurushiana risasi.
 
Alisema msako wa kuwasaka majambazi hayo, ulianza baada ya tukio hilo kutokea na kwamba tayari wamekamata Bunduki 16 zilizokuwa zimeporwa na majambazi hayo.
 
“Julai 17 zilipatikana taarifa za kuaminika kwamba maeneo ya Toangoma Mbagala, kulikuwa na majambazi waliohusika kwenye tukio la Sitakishari wakijiandaa kufanya tukio la uhalifu,” alisema na kuongeza:
“Baada ya taarifa hizo kikosi maalum kilienda eneo la tukio na kuweka mtego ili kuwanasa washukiwa.”
 
“Watu  watano waliokuwa wamepakizana katika pikipiki mbili  walisimamishwa na Polisi walikaidi kusimama na hapo ndipo  mapambano makali ya kurushiana risasi na polisi yalipoanza ambapo watuhumiwa watano walikamatwa, watatu kati yao walikuwa wamejeruhiwa vibaya na hivyo walifariki dunia wakiwa njiani kukimbizwa hospitali na watuhumiwa wawili walikamatwa na wanashikiriwa na polisi kwa mahojiano.”
 
Kova alisema Julai 19 zilipatikana habari za kuaminika kutoka kwa wasamaria wema kwamba silaha zilizoporwa kwenye kituo cha Sitakishari zimefichwa Mkoa wa Pwani katika sehemu isiyofahamika vizuri. Aliongeza kuwa vikosi mbalimbali vya Polisi vilikwenda mkoani humo na kufanya msako mkoani Pwani katika kijiji cha Mandimkongo kata ya Bupu Wilaya ya Mkuranga katikati ya msitu.
 
Baada ya taarifa za kuaminika kikosi maalumu kilifukua ardhini na katika shimo hilo zilipatikana bunduki 15 na kati ya hizo, saba ni aina ya SMG na SAR  pamoja na risasi 28. Alifafanua kuwa silaha zote zilitambuliwa kuwa zilikuwa za kituo cha  Sitakishari.
 
Alisema katika shimo hilo lillilofukuliwa ili patikana silaha moja aina ya Norinko ambayo inafanyiwa uchunguzi pia katika shimo hilo zilipatikana fedha Sh. 170,000,000 ambazo zilikuwa zimefugwa katika sanduku maalumu.
 
Watuhumiwa wa ujambazi waliouawa ni Abbas Hashimu Mkazi wa Mbagala, Yasni na Saidi wakazi wa Kitunda Kivule na wanaoshikiliwa na Polisi ni Ramadhani Hamisi (15), mkazi wa Mkuranga na Omari Amour (24) mkazi wa Mbagala.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment