Saturday, April 30, 2016

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO DOKTA MPANGO AZUNGUMZIA MASUALA MBALIMBALI BUNGENI


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango

30/4/2016
BUNGENI DODOMA
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dokta Philip Mpango, ameliambia Bunge mjini DODOMA, leo tarehe 30, Aprili, 2016, kwamba serikali inaendelea kuhakiki madeni ya walimu yaliyowasilishwa kwaajili ya malipo baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya madai hayo.

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016, serikali ilipokea madai yenye jumla ya shilingi Bilioni 29 na Milioni 800 na imelipa  20.125bn, huku madai mengine yakizuiwa baada ya kubainika hayakuwa halali.

Alitolea mfano wa mtumishi mmoja aliyewasilisha madai ya shilingi 600m badala ya shilingi laki 6, huku madai mengine yaliyolipwa miaka ya nyuma yakiwasilishwa kama madeni mapya.

Dokta Mpango alisema kuwa serikali inathamini mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini na kwamba itaendelea kulipa madai yao na watumishi wengine wa umma baada ya kuyachambua, kuyahakiki na kujiridhisha kuwa ni halali.

30/4/2016
BUNGENI DODOMA
SERIKALI imeziagiza Mamlaka ya Bandari-TPA, na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kufanya uchambuzi wa kina ili kubaini sababu za kupungua kwa shehena ya kontena zinazoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dokta Philip Mpango, ameliambia Bunge mjini Dodoma, leo tarehe 30, Machi, 2016 kwamba taarifa zilizopo zinaonesha kwamba uingiaji wa mizigo inayopelekwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Malawi na Zambia kupitia bandari hiyo, umeshuka.

Alisema katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu kontena zilizopelekwa nchini Congo zilishuka kutoka 5,529 hadi 4,092, wakati yale yaliyokuwa yakipelekwa nchini Malawi yalishuka kutoka kontena 337 hadi 265, huku yale ya Zambia yakishuka kutoka 6,859 hadi kufikia 4,448.

Hata hivyo, Dokta Mpango aliwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba kushuka kwa kiwango cha kontena ziendazo nchi jirani kupitia  Bandari ya Dar es salaam, hakujaathiri malengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alisema sababu mojawapo ya kushuka kwa idadi ya kontena zinazopitia bandari ya Dar es slaam zinachangiwa na kuporomoka kwa uchumi wa China ambao umeathiri nchi mbalimbali duniani ikiwemo  Tanzania.

"lakini naziagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA na Mamlaka ya Mapato-TRA, zichambue mwenendo huo ikilinganishwa  na nchi nyingine" alisisitiza Dokta Mpango.

Alilieleza Bunge pia kwamba, Tanzania haitozi kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kontena zinazosafirishwa kutoka bandari hiyo kwenda nchi jirani hivyo hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuzikwaza nchi jirani kutumia bandari ya Dar es salaam.

30/4/2016
BUNGENI DODOMA
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dokta Philip Mpango, amesema kuwa serikali imepanga kutumia shilingi 59.5bn kwaajili ya kuviwezesha vijiji nchi nzima katika kipindi cha mwaka fedha 2016/2017.

Dokta Mpango, aliwaambia wabunge mjini Dodoma, leo tarehe 30, Machi, 2016, kwamba fedha hizo ni kwajili ya kukiwezesha kila kijiji shilingi 50m kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali.

Alisema kuwa fedha hizo zimewekwa kwenye mfuko wa Hazina, ili kuwawezesha wadau na taasisi zitakazo husika  kupanga utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha hizo.

"Fedha hizi zitaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu" aliongeza Waziri Mpango.

Akizungumza kuhusu mikopo ya wanawake na vijana, Dokta Mpango, alisema kuwa serikali, kupitia Ofisi hiyo ya Waziri  Mkuu, imepanga kutumia shilingi 1bn kuendeleza ujuzi kwa vijana wasio na ajira na shilingi 1.955bn kuwainua wanawake kiuchumi.

Alifafanua kuwa halmashauri za wilaya, miji na majiji zitaendelea na utaratibu wao wa kutenga asilimia 5 ya mapato yao ya ndani kutoa mikopo kwa vijana na asilimia nyingine 5 kwaajili ya kuwawezesha wanawake katika maeneo yao.

Imetolewa na
Kaimu Msemaji Mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango
Simu: 0787087878

Benny Mwaipaja

No comments:

Post a Comment