Friday, September 23, 2016

KIMBISA NA BODI YAKE WAJIUZULU UHURU


WAJUMBE wa Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imejiuzulu kwa kumuandikia barua Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Adam Kimbisa.
Vyombo hivyo vya habari ni Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Gazeti la Uhuru, Mzalendo na Burudani pamoja na Peoples’ Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha Kituo cha Redio Uhuru.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli alipokea barua ya kujiuzulu kwa bodi hiyo jana.
Nakala ya barua hiyo imepelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana. Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka ilisema kuwa barua hiyo iliyoandikwa na Bodi, inaeleza kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Bodi hiyo, wameamua kwa hiyari yao kujiuzulu nafasi zao.
Wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Balozi Christopher Liundi, Nora Mkami, Tatu Abdullah, Omari Chunda, Peter Machunda na Katibu wa Bodi hiyo Gabriel Athumani.
Wajumbe wengine wanaoingia katika bodi hiyo kwa nafasi zao ni Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi pamoja na Wakurugenzi wa Redio Uhuru na Gazeti la Uhuru na Mzalendo.
Bodi ya Uhuru Media Group ndiyo yenye majukumu ya kusimamia, kuzielekeza na kuzishauri Menejimenti za makampuni hayo na kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyombo vya habari vya Chama, ambavyo ni magazeti ya Uhuru na Mzalendo pamoja na Redio Uhuru.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti nchini (RAAWU) kwa Kanda ya Mashariki, Jane Mihanji, ambaye ni mfanyakazi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, amesema kujiuzulu ni suala la kawaida na kuwa Kimbisa na bodi yake wameonesha ukomavu wa uongozi.
Amesema wiki hii Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli alitembelea ofisi za magazeti hayo na kusikiliza matatizo yanayowakabili wafanyakazi, ambayo yalikuwa ya muda mrefu na yalikuwa hayajapatiwa ufumbuzi .

amesema“Wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti alimuuliza Katibu Mkuu wa Chama (Kinana) kuwa niiondoe bodi, lakini Katibu alimueleza kuwa kuna utaratibu wa kufuatwa, hivyo kujiuzulu kwao kumeonesha ni maamuzi ya busara kabla ya kuondolewa,” 

No comments:

Post a Comment