HOSPITALI ya kisasa ya kufundishia wataalamu wa afya na kutoa huduma ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyopo eneo la kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma Januari mwakani.
Hospitali hiyo iliyojengwa kisasa kwa kutumia
mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), itakuwa ya
kwanza kutumia mfumo wa teknolojia ya sampuli hewa, unaochukua vipimo kwa
mtambo maalumu na kuwasilisha majibu kwa njia ya mtandao na itakuwa na wadi ya
watu mashuhuri akiwemo Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara
maalumu katika jengo hilo lililokamilika ujenzi wake tangu Agosti mwaka huu,
Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Ephata Kaaya, alisema hospitali hiyo,
itatoa tiba ya magonjwa yakiwemo sugu kama vile moyo, saratani na figo.
Amesema hospitali hiyo, imejengwa na kufungwa
vifaa tiba vya kisasa vya dijitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama
zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalumu kwa ajili ya kupimia
magonjwa ya wanawake, mashine maalumu za kupima na kutibu meno, koo, masikio na
pua.
“ amesemaPia tumefunga mtambo wa kisasa zaidi
wa sampuli hewa uliopo katika kila idara na kuunganishwa na maabara ambao kazi
yake ni kusafirisha vipimo na kupeleka sehemu mbalimbali na majibu ya vipimo
hivyo huwasilishwa sehemu husika kwa njia ya mtandao,”
Amesema mtambo huo, unasaidia kupunguza tatizo
la msongamano katika chumba cha maabara, unaongeza ufanisi na usahihi wa vipimo
lakini pia hupunguza muda na kuepusha mkanganyiko wa vipimo. Profesa Kaaya amesema
hospitali hiyo pia itatoa huduma za kufundishia, kufanya uchunguzi wa magonjwa
mbalimbali na tafiti za fani za afya.
Ameeleza kuwa “Lakini pia wana vyumba maalumu
12 kwa ajili ya wagonjwa wenye magonjwa ambukizi kama vile ebola, kipindupindu
na kifua kikuu,” alisema.
Amesema jengo la hospitali hiyo lina ghorofa
tisa ambazo zinajumuisha vyumba 13 vya upasuaji kikiwemo chumba kimoja cha
upasuaji kwa wagonjwa wa dharura, maabara za kisasa, vyumba vya wagonjwa
mahtuti na kusafisha figo, wodi za kujifungulia, chumba cha kuhifadhi maiti na
vyumba vya kufundishia.
Aidha amesema katika eneo la wodi zipo wodi 12
za wagonjwa mashuhuri vikiwemo vyumba viwili vyenye mitambo ya kisasa ya
kufuatilia hali ya mgonjwa vya viongozi wenye hadhi ya juu akiwemo Rais.
Profesa Kaaya, amesema ujenzi wa hospitali hiyo
uliogharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 94.5 katika eneo hilo la
Mloganzila lenye ukubwa wa ekari 3,800, ulianza tangu mwaka 2014 kupitia mkopo
wenye riba nafuu ambao malipo yake yataanza kulipwa baada ya miaka 15 kwa kipindi
cha miaka 25.
Kwa mujibu wa Profesa Kaaya, hospitali hiyo
itakayokuwa pia ya rufaa, itasaidia kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wenye
magonjwa sugu kwenda nje ya nchi kutibiwa kwani itatoa tiba na vipimo vya
magonjwa mengi sugu yanayosumbua Watanzania.
No comments:
Post a Comment