WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea hundi za thamani ya Sh milioni 140, vifaa vya ujenzi na vyakula vya thamani ya Sh milioni 32.5 kwa ajili ya kuwachangia Watanzania waliopata maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.
Akipokea msaada huo, Majaliwa aliyashukuru
makundi sita yaliyofika ofisini kwake kuwasilisha hundi hizo kwa ajili ya
kuwasaidia Watanzania hao na kusema huo ni mwendelezo wa walioguswa na jambo hilo kwa kuendelea kutoa kile
walichonacho.
Alisema wote waliochangia michango hiyo
ataiwasilisha kwa wananchi wa Kagera kwa kupitia Kamati ya Maafa ya mkoani
humo.
“Michango yote hii tutaratibu nasi tutatumia
njia yetu ya kuwashukuru kimaandishi. Kwa kupitia michango hii ndio mnaona
Kagera imetulia. Kwa niaba ya wana Kagera na Serikali tunawashukuru, muendelee
kujitokeza ili wenzetu waendelee na maisha yao kama kawaida. Mungu aendelee
kuwaongezea pale mlipotoa,” alisema Majaliwa.
Taasisi zilizowasilisha mchango huo ni Kampuni
ya simu ya Vodacom na Vodacom Foundation waliotoa Sh milioni 100, Mfuko wa
Pensheni wa LAPF (Sh milioni 20), Taasisi ya kidini ya Ahmadiya (Sh milioni
nne) na vifaa vya ujenzi vya thamani ya Sh milioni sita.
Nyingine ni Kampuni ya ujenzi ya Advent
iliyotoa tani 40 za saruji za thamani ya Sh milioni 16.5, Taasisi ya The Art of
Living Foundation iliyotoa unga wa ngano, mahindi, mchele na dawa za Sh milioni
10 pamoja na kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp linalojulikana kama
Uongozi and Leaders Forum Groups linalohusisha viongozi mbalimbali wa serikali,
viongozi wastaafu, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanahabari ambalo limetoa Sh
milioni 16.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, Septemba 10,
mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao
watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na
kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23
wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063
kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata
nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji
misaada mbalimbali.
No comments:
Post a Comment