Thursday, September 29, 2016

Wanandoa mbaroni kwa unyang'anyi




POLISI inawashikilia wanandoa kwa tuhuma za kushirikiana katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam. Wanandoa hao Bakari Abdalah (40), na mkewe Sabiha Omary(28) ni wakazi wa Vijibweni CCM, Kigamboni jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema Septemba 25 mwaka huu watuhumiwa hao walikamatwa katika doria jijini humo.
Amesema baada ya mahojiano nao walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa maeneo ya Vijibweni CCM, Kigamboni na walipofanya upekuzi walipata bastola moja aina ya Browning yenye usajili wa namba CAR A081900 ikiwa na magazini mbili na risasi tano na simu aina ya Nokia Lumia ambayo iliporwa katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha maeneo ya Mivumoni.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, Abdalah na mkewe wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio lingine lililotokea juzi saa 4.00 usiku katika maeneo ya Viwege kwa Bilal Pugu, askari wakiwa doria waliwatilia shaka watu wawili wakiwa kwenye pikipiki ambayo namba zake za usajili zimefutika.
Baada ya watu hao kuona askari wanaelekea usawa wao, mmoja aliruka katika pikipiki hiyo na kutupa begi na kukimbia na mwenye pikipiki alitoweka kwa kuendesha pikipiki yake kwa kasi kuelekea porini.
Alisema polisi walipopekua walikuta silaha aina ya SMG iliyofutwa namba zake za usajili ikiwa na magazini na risasi saba ndani yake. Hata hivyo, alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea ili kubaini matukio waliyowahi kuyafanya.
Wakati huo huo, askari wakiwa katika doria maeneo ya Tegeta karibu na shule ya sekondari ya Feza waliwatilia mashaka watu watatu wakiwa wamekaa katika kichaka na walipowaona askari walikimbia na kuacha silaha moja aina ya MARK 4 yenye usajili TZCAR 86274.

No comments:

Post a Comment