Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 , katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara. Alikuwa moja kati ya watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki. Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya babake; katika umri wa miaka 12, aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi katika shule ya msingi ya Mwisenge, iliyoko Musoma Mjini.
Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya wamisionari Wakatoliki iliyoko Tabora. Katika umri wa miaka 20, Nyerere alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
kutokana na ujasiri na nia ya kuwa mwelewa wa kila kitu ya Nyerere, Mapadre wa Kanisa katoliki wakaona akili yake na nia yake nzuri ya kutaika kujifunza wakamsaidia kusoma kozi ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.akiwa katika Chuo cha Makerere akaanzisha tawi la Umoja wa wanafunzi Watanganyika pia akaamua kujihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya sekondari ya Mtakatifu Maria (St.Mary´s), Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskoti / Uingereza akasoma Shahada ya Uzamili ya historia na uchumi, kwa hatua hiyo Mwalimu alikuwa mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.
Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam, (siku hizi Pugu Sekondari). Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika huo kikuu cha Makerere. Mwaka 1954, alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika.
Uwezo wa mwalimu uliwashitua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya. aliamua kujiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika mapigano ya uhuru.
Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Mkutano wa Baraza la udhamini (Trusteeship council) ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa kimaongezi na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na Desemba 9,1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa jamhuri ya Tanganyika. Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Hayati Mwalimu Nyerere mnamo Februari 5, 1977, aliongoza chama cha TANU katika tendo la kuungana na chama tawala cha Zanzibar ASP na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake.
Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi 1985 alipong'atuka na kumwachia nafasi rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi.
Aliendelea kuongoza Chama cha CCM hadi 1990 na kuwa makini na mfuatiliaji huku akionya katika mambo kadhaa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
baada ya kustaafu kazi ya ukuu wa nchi, Nyerere alikaa muda mwingi kijijini kwake alikozaliwa Butiama akilima shamba lake la mahindi. Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake inayojulikana kama “Mwalimu Nyerere Foundation, mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande mbalimbali wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi. Mwishoni mwa maisha yake Mwalimu aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama
Mwalimu alianza kujisikia vibaya mwezi Augost mwaka 1999, akaanza kupata matibabu ya kila mara baadae alihamishiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko Uingereza na Oktoba 14, 1999 aliaga dunia katika hospitali hiyo ambapo madaktari walisema kuwa alikuwa akisumbuliwa na kansa ya damu ( leukemia).
Leo ni miaka 17 tokea kifo chake kitokee na kugusa karibu dunia nzima hususani bara la Afrika kutokana na uongozi wake mzuri na mtu aliekuwa anapenda Amani na uwajibikaji wa watawala wa nchi mbalimbali Afrika. Hivyo watanzania inabidi tuenzi yale alioyafanya hasa kuleta uhuru wa nchi bila ya kumwaga damu, uongozi safi kwa kupinga waujumu uchumi ambao leo hii tunaona wamekuwa wengi mpaka kupelekea wananchi wetu kuwa masikini kadiri siku zinavyoenda.
No comments:
Post a Comment