Sunday, October 9, 2016

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE MKOANI SHINYANGA


Baadhi ya Watoto Wakifuatilia jambo katika Kongamano la watoto linaloendelea leo jijini Shinyanga.
Ofisa Maendele ya Jamii Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Anna Muhina akiongea na Watoto (hawapo pichani) katika kongamano la mtoto wakike linaoendelea mjini Shinyanga. 
Mkurugenzi wa Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Magereth Mussai akiongea na Watoto hawapo pichani katika kongamano la mtoto wakike linaoendelea mjini Shinyanga.

Na Mwandishi wetu, Shinyanga
KONGAMANO la mtoto wa kike lililofanyika leo mjini Shinyanga limeitaka serikali kuweka juhudi za makusudi kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia hasa kwa watoto wanaoozeshwa ndoa za utotoni kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Maadhimisho haya yanaendelea kufanyika mjini Shinyanga ili kuungana na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike inayoendelea kuadhimishwa Mkoani hapa ambayo kilele chake ni tarehe 11 Oktoba 2016.
Maadhimisho hayaufanyika kila mwaka ikiwa ni mwitikio wa Azimio la Umoja huo lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 2011.
Akiongea katika kongamano la watoto mkoani shinyanga Mkurugenzi wa Watoto Bi. Magereth Mussai kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amelaani wale wote wanaoozesha watoto ambao wako katika umri wa kwenda shule kwasababu ndoa za utotoni uwafanya watoto hawa kushindwa kufikia ndoto zao ikiwemo haki ya kupata elimu ya juu.
Wakati huo huo watoto wawili ambao hawakutaka majina yao kutajwa kwasababu ya kulinda haki za watoto wametoa ushuhuda wao wa ni namna gani ndoa za kulazimishwa wakiwa wadogo zilivyoelekea kukatiza ndoto yao kabla ya kuokolewa na shirika la AGAPE kuwaokoa
na kuwaendeleza kielimu.
Mmoja wa Watoto hao ambaye jina limeifadhiwa amesema ndoa yake ya utotoni iligubikwa na vipigo vya mara kwa mara kutoka kwa mme wake ambaye alimpatia ujauzito na baadae kumtelekeza yeye na mtoto.
Alendelea kusema kuwa inamuuma sana kama mlengwa kuwa mzazi na wakati huo kuwa mwanafunzi anayesoma kwa msaada wa mashirika yasiyo ya kiserikali huku baadhi ya wazazi na walezi wakiendeleza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.  
Watoto wao kwa pamoja wameitaka serikali na vyombo vya habari kuwekeza nguvu zao kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni ambazo zimekuwa kikwazo kwa mtoto wa kike kufikia ndoto zake.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo wasichana wapatao milioni moja wanatarajiwa kuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18 duniani kote.

No comments:

Post a Comment