Tuesday, March 7, 2017

KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI, WADAU WATAKIWA KUONGEZA FURSA ZA UCHUMI KWA WANAWAKE


Jovina Bujulu- MAELEZO.

Kila mwaka ifikapo Machi 8 kila mwaka, wanawake duniani kote  huadhimisha siku yao ambapo hujitathmini kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo walizofanya, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.

Akiongea hivi karibuni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Sihaba Nkinga alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko”

Kauli mbiu hii inasisitiza kuwajengea wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara, upatikanaji wa mitaji, masoko na biashara ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika na fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji.

“Ujumbe wa kauli mbiu hii umezingatia sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 na ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu hususani lengo namba 5 kuhusu usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi” alisema Bi Nkinga.

Kauli mbiu ya mwaka huu imetotolewa kutokana na kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN) isemayo “Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.

Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) Mama Edda Sanga alisema kuwa wanawake  wanapaswa kujiwezesha katika maeneo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii ili wapate fursa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ambayo hatimaye yatawaletea tija na mafanikio.

Hii ina maana kuwa, endapo wanawake watapata nafasi ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ni rahisi kwao kusikilizwa na hata kuwa na sauti katika masuala ya wao kumiliki ardhi, majumba na hata viwanda.

Aidha, kauli mbiu hii inawahamasisha wanawake kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa wa jinsia unaoondoa vikwazo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na kuweka ulinganifu katika ushiriki ambao unawanufaisha kiuchumi kuanzia ngazi ya familia.
Ili kufikia malengo ya kujikomboa kiuchumi, wanawake wanatakiwa kujitambua na pia kutambua malengo na mipango yao. 

Wanatakiwa kutambua na kutumia fursa vizuri wanayopata hasa mahali watakapopata taarifa za kuwanufaisha kiuchumi kwa mfano benki, vikundi vya mikopo, taasisi au hata kwa watu binafsi.

Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwakwamua wanawake kiuchumi, kutoka kwenye taasisi, mashirika na watu binafsi,  hata hivyo wao pia wanahitaji kujikomboa kwa kutumia juhudi zao binafsi kama vile kujiunga katika vikundi waweze kukopeshwa ili waweze kujiajiri katika mkondo wa uzalishaji mali, kama vile kuanzisha viwanda vidogo vidogo, kwa mfano viwanda vya usindikaji vyakula, kazi za mikono na ushonaji ambavyo havihitaji mtaji mkubwa.

Hii itawafanya kunufaika na kuondoa hali ya utegemezi katika jamii, na hivyo kujiondoa katika hali ya unyonge. 
Ni ndhahiri wanawake ndio wazalishaji wakubwa katika nyanja za kiuchumi, hivyo katika kutimiza ndoto na malengo zao ni budi juhudi zitumike ili washiriki katika kukuza pato lao na taifa kwa ujumla.

Naye Bibi Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) anasema kuwa katika kusherekea siku ya wanawake duniani, taasisi yao ilifanya  kongamano  hivi karibuni pamoja na mambo mengine walizungumzia mpango wa taifa kuhusu ushiriki wa wanawake katika kuelekea uchumi wa viwanda vya kati.

Alisema kuwa wanawake wa mjini kwa sasa wanashiriki vizuri katika shughuli ambazo huwaongezea kipato wakati wanawake  wa vijijini ushiriki wao katika shughuli za kuwaongezea kipato si wa kuridhisha kwani wanatumia muda mrefu kutembea kutafuta maji na kuni kwa ajili ya matumizi ya familia.

Bibi Liundi alitoa wito kuwa huduma za jamii zisogezwe karibu na jamii ili wanawake ambao ni wazalishaji mali wakubwa wapate muda wa kutosha kushiriki katika shughuli za kujiongezea kipato badala ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Naye Bibi Magreth Dotto ambaye ni Mhandisi wa Migodi, na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam aliwashauri watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa kuzingatia kasi ya ukuaji wa teknolojia kila siku ili baadaye wapate nafasi nzuri katika jamii na kutoa mchango wao katika kutatua changamoto za kijamii na taifa.

“Uhandisi unawezekana kwa wasichana na ni taaluma nzuri, hivyo wasichana waache kuyaogopa masomo ya sayansi, ni taaluma inayobadilisha maisha kwa kuyaboresha kwa sababu inalipa vizuri” alisema Bibi Magreth.

Kwa upande wake Dkt. Ave Maria Samakafu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo alisema kwa sasa wanawake wana mwamko mkubwa ambao umeleta mageuzi katika familia na kuinua kipato chao.

“Kwa sasa tunaona ushiriki mkubwa wa wanawake katika nyanja ya uchumi kwa sababu kuna wanawake wafanyabiashara wadogowadogo, wa kati na hata wakubwa” anasema Dkt Semakafu.

Alisema kuwa elimu inahitajika zaidi kwa wanawake wa vijijini ambao bado wanatawaliwa na tafsiri potofu ambapo ukandamizaji wa wanawake bado unapewa nafasi kubwa na jamii, hivyo kuwafanya wasisonge mbele katika kujiletea maendeleo yao.

Dkt. Semakafu aliendelea kusema kuwa wanawake wengi wa mjini wanatambua nafasi zao katika jamii, hivyo wanatumia ufahamu huo kama fursa kwao ambazo zinawasaidia katika kuleta mageuzi ndani ya familia zao.

“Vijana wa kike wamekuja na nguvu mpya, kinachoendelea sasa hivi kinafungua uelewa wa jamii, watoto na wazazi na kuwafanya watambuliwe na jamii” alisema Dkt. Semakafu. 

Dkt. Semakafu alitoa mfano unaodhihirisha nafasi ya mwanamke akimtaja Agnes Magongo ambaye hivi karibuni ameshinda tuzo ya UN ya “women economic empowerment” ambayo ni tuzo ya uwezeshaji wa wanawake.
“Wanawake tushiriki katika kuboresha maisha yetu, tusiwe wasindikizaji bali watendaji, twende pamoja katika uchumi wa viwanda ili tuweze kumiliki viwanda” alimalizia Dkt. Semakafu.

Katika kuhimiza fursa za uchumi kwa wanawake kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote nchini kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake ili waweze kushiriki na kunufaika nazo hasa kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea azma ya uchumi wa kati kwa misingi ya kuwa nchi ya viwanda.

Mama Sihaba aliwakumbusha wadau wote katika ngazi zote kuweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto zinazokwamisha kufikiwa kwa usawa wa jinsia na kusababisha wanawake na wasichana kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao kimaisha.

No comments:

Post a Comment