Thursday, May 18, 2017

WAKUU WA POLISI KUTOKA NCHI ZA SADC KUKUTANA ARUSHA.

Image result for picha ya advera
Mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la wakuu wa Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika Mei 24, 2017 mkoani Arusha chini ya mwenyekiti wa Shirikisho hilo kipindi hiki ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu. 

Mkutano huo utatanguliwa na mikutano ya kamati tendaji za SARPCCO kabla ya kufunguliwa rasmi Mei 24, 2017 na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ambapo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za pamoja katika kubaini na kukabiliana na makosa mbalimbali yakiwemo dawa za kulevya, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na ugaidi. 

Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi mjini Bagamoyo. 

Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo. 

SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Shirikisho hilo linaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Syshelis. 



Imetolewa na:- 
Advera Bulimba-ACP 

Msemaji wa Jeshi la Polisi. 
Makao Makuu ya Polisi.

No comments:

Post a Comment