Akitoa uamuzi wa shauri hilo mjini Kigoma, mwamuzi wa shauri hilo, L.L Mwakyusa alisema baada ya mlolongo mzima wa uamuzi wa pande zinazohusika, Tume imeamua kuwa walalamikaji si wanachama wa CWT tena na kitabaki kuwa wakala kwa walalamikaji kwa kuwa ni chama pekee kinachotambuliwa na mwajiri.
Aidha, Mwakyusa alisema suala la makato kwa walimu hao linapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa pande hizo zimeshaingia kwenye mgogoro na kwamba walimu hao hawatafaidi matunda halisi kama wanachama.
Pamoja na uamuzi wa kujitoa kwa walimu hao na kujiunga na chama kingine, alisema walimu hao wataendelea kukatwa ada ya uwakala ili kufaidi matunda ya masuala ya jumla kama walimu yatakayosimamiwa na CWT kwa mujibu wa kifungu cha 72 (c) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004.
Akizungumzia hukumu hiyo, kiongozi wa kundi hilo la walimu, Kalimwabo Sabibi alisema pamoja na Tume hiyo kuridhia kujitoa CWT, wanakusudia kuanzisha chama kingine cha walimu kitakachosimamia maslahi yao.
Sabibi alisema kwa muda mrefu, walimu wamekuwa kama watoto yatima kutokana na CWT ambacho machoni kinaonekana kama kinasimamia maslahi yao, kudai hakifanyi chochote kwa ajili ya maslahi ya walimu.
Alisema walimu wamekuwa kwenye malumbano ya kudai maslahi yao kutoka kwa mwajiri badala ya chama hicho kuwa upande wao, wakati mwingine kimechangia kuwafanya wakose hata kile kidogo wanachodai.
Pamoja na hukumu hiyo, hata hivyo walimu hao wamesema hawajaridhishwa na uamuzi wa Tume kuruhusu kuendelea kukatwa kwa makato kutoka katika mishahara yao kwa ajili ya kuchangia CWT kwa kigezo cha ada ya uwakala wakati wao si wanachama wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment