Tuesday, May 22, 2012

Majambazi wavamia, wapora Uhasibu Arusha







MAJAMBAZI zaidi ya 20 wakiwa na silaha za jadi na moto, usiku wa kuamkia jana walivamia Chuo cha Uhasibu (TIA) kilichopo Njori nje kidogo na Jiji la Arusha na kupora vitu mbalimbali vinavyosadikiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 19.

Habari kutoka chuoni na kuthibitishwa na polisi mkoani Arusha, zilieleza kuwa uvamizi huo ulifanyika saa 8 usiku na majambazi hao waliingia chumba kimoja baada ya kingine na kupora vitu hivyo bila ya kudhuru mtu.
 
Rajabu Lingoni mwananfunzi wa chuo alisema hawakuwa na namna ya kujinusuru kwani watuhumiwa hao wa ujambazi walikuwa wengi kupindukia.

Lingoni alisema mbali ya kuwa wengi pia walikuwa na silaha mbalimbali, ikiwamo silaha za moto na silaha za jadi zikiwamo panga, sime, mikuki na marungu makubwa na walikuwa wakisikika wakisema yeyote mwenye kupiga simu, cha moto atakiona hatua iliyowafanya wanafunzi kukubali matokeo yoyote.

Alisema vitu walivyoporwa ni kompyuta 27, simu za mkononi aina mbalimbali zaidi ya 50, viatu jozi zote karibu za wanafunzi wote wa chuo hicho, vyote vinakadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 19.

Mwanafunzi huyo alisema baada ya kufanya uhalifu huo, majambazi hao waliondoka na kuacha mkwara mzito uliowafanya kutopiga simu usiku huo polisi na hadi asubuhi walipowasiliana na polisi na kutoa taarifa hiyo.

“Hapa tulipo sasa tuko na polisi na wanafanya uchunguzi wao, lakini wanafunzi wote wamesikitishwa na hali hiyo iliyojitokeza na kuwafanya kurudi nyuma sana kutokana na vitendea kazi vilivyoibwa kwani tuliamrishwa kulala chini bila ya kupiga kelele na wao kuendelea kukusanya wanachotaka,” alisema.

Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Thobias Andengenye alikiri kuwapo kwa uhalifu huo na kuahidi kutoa taarifa rasmi leo.

Hata hivyo, kuingia kwa kundi hilo la majambazi chuoni hapo, kunatia shaka kwani kinalindwa na askari wa kampuni za ulinzi na haijulikani walikuwa wapi wakati majambazi hao wakiingia ndani na kufanya uhalifu huo.





No comments:

Post a Comment