Tuesday, May 22, 2012

Nassari akemea uvamizi wa mashamba ya wawekezaji


MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amewataka wakazi wa Arumeru kuacha kuvamia mashamba ya wawekezaji bila mpango, bali kuwa na maono ya jinsi ya kuyaendeleza aidha kwa kujenga shule au hospitali, na sio kuyagawana na kuyauza kwa watu.

Aliyasema hayo wakati wa Ibada ya Shukrani iliyofanyika kwenye Kanisa la FPCT Kilinga akimshukuru Mungu kwa kumwepusha na majaribu mbalimbali na hatimaye kushinda ubunge.

Mbunge huyo wa Chadema alisema uchaguzi umemalizika na sasa kilichopo ni kufanya kazi za wananchi na hivyo yuko tayari kushirikiana na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuleta maendeleo na kuahidi kwamba wale watakaokwamisha jitihada hizo watashughulikiwa.

lisema ana kila sababu ya kumshukuru Mungu, kabla ya kwenda kutembelea wananchi katika kila kata kuwashukuru na ili kujiweka karibu zaidi na Mungu, ameamua kuanza kutoa sadaka kanisani kwanza.

Pia alitumia nafasi hiyo kanisani kuwaomba wananchi, kutembelea ofisi ya Mbunge ili kutoa kero zao, kwa ajili ya kumwezesha kuziwakilisha bungeni.

Nassari akiwa amesindikizwa katika sadaka yake hiyo ya shukrani na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) huku Deo Filikunjombe (Ludewa- CCM) na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), wakishindwa kuja na kuahidi kutuma sadaka yao ya shukrani baadaye, aliwashukuru kwa ushirikiano wao.

Kwa upande wake, Mchungaji Langael Kaaya alilitaka taifa kuepuka kuchagua viongozi wanaotumia rushwa katika uchaguzi, ambao wakishinda badala ya kunufaisha Watanzania kwa rasilimali zilizopo, wanazitumia kwa manufaa yao wenyewe.

Mchungaji Kaaya alisema taifa lilipofika kwa sasa, linalazimika kupata viongozi wasio na mapenzi na wananchi kwa sababu ya rushwa.

Alisema rushwa inatumika kuharibu na kupoteza haki, pamoja na kuharibu mipango ya Mungu, hata pale wananchi wanapohitaji kufanya mabadiliko, hayafanyiki na yanavurugwa na rushwa.

Aidha, aliomba watu kufunga na kukataa dhambi ya mauaji, inayofanywa na baadhi ya watu katika eneo la Meru, ya kuuwa watu kwa kuchinja na kuwanyonga hasa baada ya kumalizika Uchaguzi Mdogo wa ubunge, ili Mungu awasamehe dhambi hiyo na vizazi vyao.

 
     

 
J
     
 
 

No comments:

Post a Comment