Sakata
la walimu kutangaza azma ya kugoma limeendelea kushika kasi ambapo
walimu katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wamesema wako tayari
kukatwa mishahara yao iwapo serikali itaona hiyo ndiyo njia sahihi ya
kuwazuia wasigome.
Akitangaza azma hiyo wakati wa kikao cha
makubaliano ya kuungana na wenzao nchi nzima kushiriki mgomo huo, Katibu
wa Chama cha walimu wilayani humo, Josephat Mashinji, alisema ofisi
yake ilipokea waraka wa mgomo kwa nchi nzima tangu Mei 13, mwaka huu.
Alisema kuwa waraka huo umetoa notisi ya
siku 30 hadi Julai 8, mwaka huu kuitaka serikali itekeleze matakwa yao
mbalimbali vinginevyo wataitisha mgomo usio na kikomo kwa nchi nzima.
Alisema kwa kuzingatia waraka huo wako
tayari kukatwa mishahara yao katika kipindi chote cha mgomo iwapo
serikali itaona ndiyo njia sahihi ya kuzuia mgomo huo. Alisema hatua
hiyo inatokana na ukweli kuwa hivi sasa wanatambua haki zao za kikatiba
na wako tayari kuzipigania.
Kwa mujibu wa Mashinji, hivi sasa CWT kipo
katika mgogoro na serikali utakaodumu hadi Julai 8, mwaka huu, na
endapo serikali haitaridhia, chama hicho kitatangaza mgomo wa walimu
kutokwenda kazini.
Miongoni mwa madai yao, walimu wanataka
nyongeza ya mshahara kwa asilimia100, asilimia 55 ya posho kwa walimu wa
masomo ya Sayansi, asilimia 30 kwa walimu wanaofundisha katika
mazingira magumu na asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya sanaa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment