Thursday, June 7, 2012

Kumi waliokufa ajalini Mbeya watambuliwa






MIILI ya watu kumi kati ya 13 waliofariki katika ajali iliyotokea juzi mkoani Mbeya imetambuliwa na ndugu zao.Taarifa za Jeshi la Polisi zimethibitisha kutambuliwa kwa miili hiyo na kueleza kuwa miili mingine ya watu watatu  bado majina yao haijambuliwa.

Maofisa wa polisi, ambao hawakuta kuandikwa majina yao kwa walichodai kuwa wao si wasemaji wa jeshi hilo wametaja majina ya marehemu hao kuwa ni Lucia Livingston (51),mkazi wa Kutumba wilayani Rungwe, Erenesta Kikanga (62), mkazi wa Ifunda mkoani Iringa, Emmanuel Mwanjanje mkazi wa Ilomba jijini Mbeya na Pius Mbeye mkazi  wa Uyole.


Wengine ni Mwase Pius mkazi wa Iganjo Mbeya, Uzuri Ngomano (49), mkulima wa Isongole wilayani Rungwe, Bahati Jafari (33) mkazi wa Kyela na Mwaniwe Fokasi (35) mkazi wa Uyole.

Walisema kuwa wengine waliotambuliwa ni Mwasa daimoni (32), mkazi wa Ilomba jijini Mbeya  ambaye alikuwa dereva wa Coaster na Yerusalem Mwakyusa(35).

Miili ya marehemu hao iliyokuwa imehidhifiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, imechukuliwa na ndugu zao na ksafirishwa kwa mazishi baada ya kutambuliwa.

Hata hivyo, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Thomas Isdory , alisema kuwa kati ya majeruhi 16, tisa walitibiwa na kuruhusiwa siku hiyo ya ajali baada ya hali zao kuwa nzuri huku majeruhi wengine saba wakilazwa hospitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri.

“Kati ya majeruhi 16, majeruhi tisa walitibiwa na kuruhusiwa siku hiyohiyo, wengine saba walilazwa baada ya hali kuwa mbaya. Lakini tunamshukuru Mungu hadi sasa wanaendelea vizuri,”alisema.

Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kuwaona majeruhi waliolazwa na kuzungumza nao ambapo pamoja na hali zao walieleza kuwa wanamshukuru Mungu pia madaktari waliopa matibabu hadi sasa wanaendelea vizuri.

“Tunamshukurui Mungu, kwa kweli hadi sasa naendelea vizuri japo kuwa bado nina maumivu kigogo mwilini, hasa kwenye mbavu ambako nilijigonga sana. Lakini pia, nawashukuru madaktari kwa jitihada zao kuokoa maisha yangu,”alisema majeruhi aliyejimbulisha kwa jina la Fold Mwakabungu.

Ajali hiyo ilitokea eneo Igawilo katika  Mlima Mzalendo nje kidogo ya Jiji la Mbeya, ambapo imeelezwa kuwa eneo ni maarufu kwa ajali.

No comments:

Post a Comment