Sunday, June 24, 2012

Mkurugenzi Arusha akamatwa na Takukuru

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Jiji la Arusha, Raphael Mbunda (51) na wenzake watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa shitaka la kuhujumu uchumi, kwa kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia hasara serikali baada ya kuipatia tenda, kampuni ya Luneco Investment Company Limited, kinyume cha sheria.

Washitakiwa wengine ni aliyekuwa Mweka hazina wa Manispaa hiyo, Christopher Mbalakai (37), Mwansheria wa Manispaa hiyo, Paulo Mugasha (45) na Mkurugenzi wa kampuni ya Luneco Investment Company Limited, Nestory  Ng’hoboko.



Akisoma mashitaka hayo mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hangi Chang’ah , mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Gantwa Mwanguga, alidai kuwa washtakiwa hao wameshitakiwa kwa makosa manne, ambapo shitaka la kwanza hadi la tatu linawahusu washitakiwa watatu tu.


Mwendesha mashitaka huyo alisema shitaka la kwanza Mkurugenzi huyo na wenzake ambao ni mweka hazina na mwanasheria,  wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, kati ya mwaka 2008 na 2010 kwa siku toauti, kwa kumkaribisha mdhabuni wa kampuni ya Luneco Investment Company Limited bila  kufuata taratibu za utoaji tenda na kuvunja sheria.

Shitaka la pili ilidaiwa kuwa washitakiwa hao wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka  waliyofanya Agosti 23 mwaka 2010 kwa kuruhusu  tenda kwa kampuni hiyo ya kukarabati eneo la maegesho ya magari na bustani huko Kijenge manisapaa ya Arusha, kinyume cha sheria.

Chang’a alisema kuwa shitaka la tatu washitakiwa hao, walitenda kosa lingine Agosti 23 mwaka 2010 kwa kuipatia kazi kampuni ya Luneco Investment Company Limited  ambaye alijiptia sh milioni 45.7 wakati hakustahili kuzipata.


Shitaka la nne lilisomwa kwa washitakiwa wote wanne, ambapo ilidaiwa walitenda kosa Agosti 23,  2010 na Septemba 2010, walishindwa kusimamia kazi hiyo na kusababishia serikali hasara ya Sh milioni  25.5

Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana, ambapo kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye mali ya shilingi milioni tano na  kitambulisho na mshitakiwa wanne alitakiwa kuwa na mdhamini mwenye mali isiyohamishika ya shilingi milioni tano na alitimisha masharti hayo na wote wapo nje kwa dhamana hadi kesi itakapotajwa tena Julai 19 mwaka huu.


No comments:

Post a Comment