Mshirika mkuu wa aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo amekamatwa nchini Togo na kurudishwa nyumbani.
Moise Lida Kouassi ni wa kwanza kati ya
washirika wa Bwana Gbagbo kukamatwa kwa kuhusika na mgogoro wa mwaka
jana uliofuatia uchaguzi wa mwaka 2010.Hali hiyo ilifuatiwa na mvutano wa miezi minne ambapo alikataa kumkabidhi madaraka Alassane Ouattara, aliyeshinda uchaguzi huo.
Bwana Gbagbo hivi sasa yuko mjini The Hague akisubiri kesi kwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa mgogoro huo.
Hati ya kumkamata Bwana Kouassi, aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi wa Bwana Gbago pamoja na wengine 23 ilitolewa mnamo Juni 2011.
Hatua ambayo haikutarajiwa
Mwandishi wa BBC mjini Abidjan anasema Bwana Kouassi alitoka kwenye ndege Jumatano usiku akiwa amefungwa pingu na akionekana kama aliyepigwa na mshangao kuona amerudi nyumbani.
Aliwasili saa chache tu baada ya Rais Ouattara, ambaye alikua mji mkuu wa Togo,Lome, kuhudhuria mkutano .
" Nadhani kila mtu anamfahamu Bwana Lida Kouassi na kuhusika kwake katika kila kitu kilichotokea nchini mwetu katika kipindi cha miaka 10 iliopita," Alisema Rais Ouattara .
Kouassi anazuiliwa katika mtaa wa kibiashara wa Plateau mjini Abidjan na anatazamiwa kuhojiwa na jopo la majaji kuhusu jinsi alivyochangia katika ghasia zilizoitikisa nchi ya Ivory Coast mwaka jana.
Bwana Kouassi alikuwa waziri wa ulinzi wakati wa jaribio la mapinduzi la Septemba 2002 kugeuka uasi na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo maelfu waliuawa na nchi kugawanyika Kaskazini na Kusini.
Katika miaka michache iliyopita hakushikilia wadhifa wowote rasmi lakini alikuwa ni mmojawapo wa washauri wa Gbagbo na wachambuzi wa kisiasa wanamchukulia kama mtu mwenye msimamo mkali.
Washirika wengine kadhaa wa Bwana Gbagbo nao pia wanaishi uhamishoni Afrika Magharibi,mkiwemo Ghana na Benin.
No comments:
Post a Comment