Friday, June 8, 2012

IMF kurejesha ufadhili kwa Malawi



Maandamano kupinga uhaba wa mafuta Malawi
Shirika la Fedha Duniani IMF limesema kwamba litatoa dola milioni 157 kama mkopo kwa Malawi ili kuuchepua uchumi wake ambao umedorora.Malawi imekuwa na matatizo ya uchumi wake tangu IMF kukatiza ufadhili wake mwaka jana.
Rais wa zamani Bingu wa Mutharika ambaye alifariki dunia hapo mwezi Aprili alikosolewa vikali na jamii ya kimataifa kwa ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na kutoweka misingi imara ya ukuaji wa uchumi.
Mrithi wake, Rais Joyce Banda amefanya mabadiliko kadhaa ambayo yanaungwa mkono na wafadhili. Malawi ni moja wapo wa nchi masikini zaidi duniani na ufadhili wa nje unachangia kwa kiwango kikubwa bajeti yake.
Mwezi jana Bi Banda alishusha thamani ya sarafu ya nchi hiyi 'Kwacha' hatua iliyopingwa na Wa Mutharika licha ya shinikizo kutoka kwa IMF. Pia Rais mpya ameweka huru biashara ya kubadilisha fedha za kigeni.
Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani nchini Malawi Tsidi Tsikata, amesema mkopo huo tayari kuidhinishwa na bodi ya IMF. Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani Banda ameonyesha ari kuhakikisha nchi yake inarejeshewa ufadhili baada ya kukumbwa na uhaba wa mafuta na sarafu za kigeni.
Baadhi ya nchi za magharibi zimetishia kukata ufadhili endapo Malawi haitaheshimu haki za wapenzi wa jinsia moja. Wiki jana Uingereza ilitangaza dola milioni 50 kama msaada kwa Malawi.

No comments:

Post a Comment