Mtoto huyo, Issa Hassan achomwa mikono yote
Mtoto huyo, Issa Hassan anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Twiga, Mtoni Kijichi, amelazwa katika Hospitali ya Temeke baada ya hali yake kuelezwa kuwa mbaya baada ya kupata majeraha makubwa ya moto huo.
Akiongea kwa shida hospitalini hapo, mtoto huyo alisema unyama huo alifanyiwa majira ya saa 5:00 usiku eneo la Mtoni Kijichi na mama yake huyo aliyefahamika kwa jina la Fatuma Yusufu (52), ambapo imeelezwa kabla ya kuunguzwa kwa moto huo alilazimishwa kufanya mazoezi ya kushika masikio.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio zinaeleza Issa alichukuliwa na mama yake mkubwa kutoka Mtwara akiwa bado mdogo kwa ajili ya kumlea baada ya mama yake mzazi kuugua maradhi ya akili kwa siku nyingi.
Alisema siku ya tukio mama yake alimfuata kwenye chumba anacholala na kumuuliza kama amechukua sh 500 za mauzo ya biashara yake ya samaki wa kukaanga. Hata hivyo, alimjibu hakuchukua pesa hiyo, lakini mama yake alipinga na kusisitiza kuzichukua.
"Alinisubiri wakati wa kulala alikuja na kuniuliza kama nilichukua Sh 500, nilikataa lakini alionekana kuwa mkali huku akisema nimechukua," alisema mtoto huyo.
Wakati wa majibizano hayo yakiendelea, Fatuma alimkamata na kumshurutisha kupiga magoti na ashike masikio kama moja ya mazoezi.
"Mama aliniambie nipige magoti nianze kufanya mazoezi ya kushika masikio, baadae aliniambia nikae chini na ninyooshe miguu yangu," aliendelea kusema.
Baada ya kutii amri hiyo alimkamata mikono yake na kumfunga matambaa na mifuko ya nailoni. Alipohakikisha hawezi yameenea mikono yote alichukua mafuta ya taa na kisha kumwagia kabla ya kumuwasha kwa kibiriti.
Moto ulivyokuwa ukiwaka mtoto huyo alilia kwa uchungu kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyasikia, kitu ambacho kilisababisha majirani kujitokeza na kuanza kumuokoa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Aminajat Kilema ambaye amejitolea kumuuguza mtoto huyo hospitalini hapo, alisema kutokana na maelezo ya majirani walidai wakati wa kumuokoa mtoto huyo ilibidi watumie nguvu kutokana na mwanamke huyo kumng'ang'ania akitaka moto huo uendelee kumuunguza hadi uzimike wenyewe.
"Majirani walijitahidi kumuokoa kwa taabu sana, alikuwa mkali na ilibidi kutumia nguvu kubwa kumchukua mtoto na kuuzima moto, lakini tayari alikuwa ameungua vibaya," alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Amani Malima alisema walimpokea mtoto huyo juzi akiwa katika hali mbaya baada ya moto kuunguzwa mikono yake kwa asilimia hamisini. Hata hivyo baada ya kumpati matibabu hali yake imezidi kuimarika.
Taarifa zilizopatikana wakati Gazeti hili linakwenda mitamboni kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Temeke Sultan Mziray alieleza idara yake kwa kushirikiana na jeshi la Polisi imemfikisha Fatuma katika Mahakama ya mfawidhi Wilaya ya Temeke kujibu tuhuma hizo.
Hata hivyo, imeelezwa licha ya mtoto huyo kupewa matibabu, anakabiliwa na matatizo kadhaa ikiwa pamoja na ukosefu wa mavazi na chakula baada ya kutokuwa na ndugu jijini.
Aidha kwa watu watakaoguswa na mkasa wa mtoto huyu na kutaka kutoa msaada wa haraka wanaombwa kufika ofisi ya Ustawi wa jamii Wilaya ya Temeke au wawasiliane kwa simu namba 0712481919.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment