Monday, July 9, 2012

Balozi: Kiswahili kiwe lugha ya biashara EAC

Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutisa
Wafanyabiashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wametakiwa kukienzi Kiswahili ikiwa ni lugha muhimu ya biashara zao na bidhaa zao ziwe kwenye maandishi ya lugha hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutisa, wakati wa mkutano wa siku moja wa mahusiano ya kitaaluma kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya wale wa sekta binafsi.

“Kiswahili kilianza Tanzania, kikafika Kenya kikapata homa, kufika Uganda tu kikalazwa, Rwanda kikapelekwa ICU lakini kilipofika Burundi kikazikwa,” alisema balozi huyo huku akishangiliwa na wafanyabiashara hao wengi wao wakiwa ni kutoka Kenya. Aliwataka wafanyabiashara hao kuachana na tabia ya kukionea haya Kiswahili kwani ndio lugha pekee ya kujidai nayo mtu anapojiita mwana Afrika Mashariki.
Balozi huyo alisema wafanyabiashara wa mataifa mengine wanaona sifa na fahari wanapotumia lugha yao kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya biashara. Lakini pia alisisitiza kuwa hata lugha wanazotumia wafanyabiashara wa mataifa hayo ambazo hutumika kweye bidhaa zao, Afrika mashariki nao wanaiga kwa kuweka lugha hizo.
Aliwataka wafanyabiashara hao kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria za nchi husika kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wadau wazuri na serikali zinazounda jumuiya hiyo.
Balozi Mutisa alisisitiza kuwa wakati wafanyabiashara hao wakihitaji huduma serikalini, lazima nao wajue wajibu wao kwa serikali hasa kwa kulipa kodi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, alisema lengo kuu hasa la mkutano huo, ni kujadili ni kwa nini biashara zinazofanywa kati ya nchi hizo mbili haziendelei na mbali na wafanyabiashara wenyewe kutokuwa na mafanikio, lakini wananchi ni maskini wa kutupwa.
“Biashara zinafanywa, sheria zipo, kanuni zipo lakini kwa nini biashara hazikui. Watu wetu wanaendelea kuwa maskini na mitaji haikui…” alisema.
Akizungumzia biashara kwa upande wa Tanzania, alisema kumekuwa na vikwazo vingi ambavyo si vya kisheria.
Alitoa mfano kuwa nchini Kenya unaweza kupata bidhaa za Tanzania lakini Tanzania huwezi kuzikuta bidhaa fulani za Kenya, hali aliyodai kuwa inatokana na vikwazo hivyo ambavyo si vya kisheria.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kukiwepo na fursa nyingi za uwekezaji nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla, umaskini utatoweka kwa kuwa soko la ajira litaongezeka zaidi kwa wakazi wake wapatao milioni 139.
Mkutano huo wa siku moja umeshirikisha wafanyabiashara kutoka Kenya na wenyeji Tanzania lakini na maofisa waandamizi wa Mamlaka za Mapato za nchi hizo na wataalamu wengine.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment