Jeshi
la polisi mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu 18 wenye umri kati ya
miaka 18-20 kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu za mgomo wa madereva
wa daladala waliokuwa wanapinga ongezeko la ushuru.
Kaimu Kamanda wa mkoa wa Kilimanjaro, Koka
Moita, alisema watu hao wanasadikiwa kuwa ni vibaka waliojitokeza
wakati wa mgogoro huo kwa lengo la kujipatia maslahi yao binafsi.
Alisema, kutokana na vurugu hizo, magari
mawili yaliharibika na watu watatu waliokuwa kwenye gari namba T 703
AGQ walijeruhiwa na kupelekwa hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.
Imedaiwa kuwa vijana hao walikuwa
wakifanya fujo zikiwemo kuwashusha abiria kwenye magari ambayo yalitii
amri ya manispaa ya ongezeko la ushuru na kuwachapa viboko.
Hata hivyo, Moita alisema, kabla ya
ongezeko hilo daladala zilikuwa zinalipa Sh. 1000, na mabasi Sh 1500
kama ushuru wa maegesho lakini kwa sasa katika sheria iliyopitishwa na
manispaa iliwataka kulipa Sh 1500 kwa daladala, na Sh 2000 kwa magari
makubwa, jambo ambalo lilileta mgogoro mkubwa.
Kaimu kamanda alisema kuwa, jeshi la
polisi haliusiki na kitu chochote katika mgogoro unaoendelea kati ya
manispaa na wadau wa usafi, lakini wataendelea kuweka doria ili
kuhakikisha hakuna vurugu yoyote inayoendelea mpaka muafaka
utakapopatikana.
No comments:
Post a Comment