Monday, July 9, 2012

Ulinzi Shirikishi wapunguza uhalifu nchini

Jeshi la Polisi limesema kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makosa ya uvunjaji nyumba yaliyokithiri nchini.

Hayo yalisemwa juzi na Kamishina Msaidizi wa jeshi hilo, Rashid Seif wa kitengo cha kuzuia uhalifu wakati akizungumza na waandishi katika maonyesho ya 36 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

Alisema ulinzi shirikishi ni jambo muhimu kwa kuwa umesaidia kuleta mafanikio katika jamii ambapo kila wananchi ana wajibu wa kulisimamia suala hilo badala ya kuwaachia vyombo vya dola peke yao.
Hata hivyo, alisema changamoto iliyoko kwa sasa ni viongozi wa kata na tarafa kutoa elimu kwa jamii ili waache kujichukulia hatua.

Alisema wananchi bado wamekuwa wakijichukulia sheria badala ya kuviachia vyombo vya dola kuwawajibisha watakaokutwa na hatia.

"Bado elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi ili waache kujichukulia hatua pindi wanapokutana na wahalifu utakuta mtu ameiba watu wanampiga hadi anafariki hivyo haitakiwi waiachie vyombo vya dola vichukue hatua," alisema

Alisema pia ulinzi shirikishi imesaidia kupunguza kesi mbalimbali katika vituo vya polisi, hivyo jamii inatakiwa kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha nchi inakuwa katika amani na utulivu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment