Jarida
la The African Report, limefichua dili la serikali la kuimilikisha
ardhi yenye ukubwa wa hekari zaidi ya 300,000 kwenye Bonde la Mto Rufiji
lililoko mkoani Pwani kwa kampuni ya Muasia wa Bangalore inayojulikana
kama Karutari Global.
Jarida hilo limeripoti kuwa mwekezaji huyo anatarajiwa kujipatia hekari hizo iwapo mipango hiyo inayojadiliwa itakwenda vizuri.
Kadhalika jarida linasema Tanzania
inaongoza barani Afrika eneo la Kusini mwa Jangwa Sahara kwa kumilikisha
kiasi kikubwa cha ardhi yake kwa wawekezaji wa kigeni na kwamba hadi
sasa imetoa hekari zaidi ya milioni moja za maeneo yenye rutuba kwa
wawekezaji wa nje.
Habari za kuuza ardhi ya Afrika
zimechapishwa kwenye jarida hilo toleo namba 41 la Julai 2012, lenye
kichwa cha habari toleo maalumu “Namna wanasiasa walivyoachia Dola
bilioni 100 za ardhi. Taarifa maalumu ya uchunguzi wa siri ya dili
anayotishia mamilioni ya wakulima wa Afrika.”
Ripoti maalumu iliyochapishwa kurasa za 23
na 24 za jarida hilo inaitaja Tanzania kuwa imeuza hekari 1,083,000 za
ardhi kuanzia mwaka 2006 na kuanika kuwa watuhumiwa wa ufisadi huo wa
ardhi ni
wanasiasa na viongozi wa serikali ambao hugawa ardhi ya taifa
kwa wageni kwa kuingia ubia na wageni .
“Wakati mwingine wanajichukulia ardhi bila
kufuata taratibu na sheria zilizopo. Huwahonga viongozi wa vijiji na
kuwashinikiza kuitisha mikutano ya haraka inayowezesha kutimiza azma
hizo,” jarida hilo likimkariri Barnaba Baha wa asasi ya kimataifa ya
Action Aid.
Ripoti inasema kwenye bonde la Mto Rufiji
mpango wa kuuza zaidi ya hekari 300,000 unaendelea na kuitaja kampuni ya
India ya Karutari Global iliyowekeza nchini Ethiopia kuwa ndiyo
inayokusudiwa kupewa eneo hilo.
Jarida linaeleza kuwa Karutari Global ni
kampuni ya Bangalore inayomilikiwa na Muasia Sai Ramakrishna Karutari
aliyeelezwa kuwa ni mmiliki wa majumba ya kuendesha kilimo (green house)
yanayozalisha miche zaidi ya milioni 650 za maua ya rozi kila mwaka .
Jarida linawakariri wasemaji wa Benki ya
Dunia (WB) wakishangaa uuzaji huo wa ardhi kwa kile wanachokiita ni dili
dhidi ya maili za mraba milioni 1.5 za ardhi ambazo hazijaguswa lakini
sasa zinatolewa kwa wawekezaji wa kigeni na tawala za Kiafrika.
Watafiti wanaeleza kuwa uporaji huu wa
ardhi ni aina nyingine ya kugombea Afrika kama ule uliofanyika mwaka
1885 baada ya mkutano wa Berlin ulioigawa Afrika kwa wakoloni ambapo
Tanganyika ( sasa Tanzania ) ilichukuliwa na Wajerumani.
Mtafiti kutoka Ethiopia akizungumzia kiama
cha wakulima wa Afrika alikaririwa na jarida hilo: “Ninasema
kinachotokea barani Afrika ni kuigombea Afrika lakini kwa hili la sasa
ni serikali zenyewe kupora ardhi za watu wake na kuwazawadia
wawekezaji.”
Kama kawaida jarida hilo linaeleza kuwa
viongozi wa Afrika wameendelea kuimbiwa nyimbo za hadaa kuwa uwekezaji
utaleta ajira kwa vijana, utaboresha teknolojia ya kilimo na kuongeza
uzalishaji utaokaopunguza umaskini.
Habari hizo zinaitaja Tanzania, Kenya,
Zambia, Uganda, Kongo , Ethiopia, Mali, Msumbiji na Liberia kuwa
zinaonyesha sura ya serikali za Afrika zinavyojizatiti kuvutia mitaji ya
nje kwenye sekta ya kilimo.
Hata hivyo jarida linaeleza kuwa cha
kushangaza mipango ya kujitwalia ardhi za wakulima pembezoni hufanywa
kwenye miji mikuu bila kuwashirikisha wakulima wamiliki ambao ndiyo
wahanga wa uporaji huo.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment