Saturday, July 7, 2012

Madikteta wa Argentina wakutwa na hatia ya kuiba watoto

Dikteta wa zamani wa Argentina Jorge Rafael Videla amehukumiwa kifungo cha miaka 50 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuwaiba watoto wa wafungwa waliotekwa nyara na kuuwawa wakati wa vita vya utawala wa kijeshi dhidi ya wapinzani wa chama cha mrengo wa kushoto, miongo mitatu iliyopita.

 Dikteta wa mwisho kuitawala Argentia Reynaldo Bignone  pia alipatikana na hatia na kupewa kifungo cha miaka 15 jela. Tayari madikteta hao wako gerezani kwa hatia nyingine za uvunjaji wa haki za binadamu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema huenda watoto wapatao 500 waliibiwa kati ya mwaka 1976 na 1983, lakini ni vigumu kuhakikisha kwa sababu ya kuharibiwa kwa nyaraka, na muda mrefu uliopita.


 Kulingana na utaratibu wa mahakama nchini Argentina, ushahidi uliotumiwa kuwapata na hatia madikteta hao utabakia kuwa siri hadi tarehe 17 Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment